DKT. SAMIZI ATAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI UJENZI WA JENGO LA TIBA YA SARATANI KWA NJIA YA MIONZI
Posted on: March 5th, 2026Na Shaban K. Juma, WAF-Mbeya
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amemtaka mkandarasi anayejenga jengo la tiba ya saratani kwa njia ya mionzi (Radiotherapy) kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa ukanda husika
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Machi 04, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ya afya pamoja na hali ya utolewaji wa huduma katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya, ambapo ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawawezesha wagonjwa wa saratani kupata matibabu ya mionzi karibu na makazi yao badala ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Dkt. Samizi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika kuimarisha huduma za matibabu ya saratani nchini, hivyo ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa viwango na muda uliopangwa.
Amesema huduma ya tiba ya saratani kwa njia ya mionzi ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa matibabu, kupunguza gharama kwa wagonjwa na familia zao, pamoja na kupunguza msongamano katika hospitali nyingine za rufaa. Aidha, ameihakikishia jamii kuwa Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ili kuhakikisha huduma bora na za kibingwa zinawafikia wananchi wote kwa wakati.