Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

“ASILIMIA 86 YA WATU WENYE UMRI WA MIAKA 18 NA KUENDELEA WAMEPATA DOZI KAMILI YA CHANJO YA UVIKO-19” - WAZIRI UMMY MWALIMU

Posted on: January 19th, 2023

Na E.Kayombo, WAF – Dodoma.

Kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Mwezi Julai hadi Desemba 2022 Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya wamefanikisha utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kufikia asilimia 86 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kupata dozi kamili ya chanjo dhidi ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu leo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Afya kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Desemba 2022 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Jijini Dodoma.

“Ndani ya miezi sita tumefanya vizuri kwenye utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19, tumeweza kufikia asilimia 86 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kupata dozi kamili ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 ukilinganisha asilimia 24.7 hadi kufikia mwezi Juni, 2022” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Amesema kuwa hadi kufikia Desemba 31, 2022 jumla ya dozi 46,848,520 zilikuwa zimepokelewa ambapo dozi 41,581,670 zilikuwa zimesambazwa nchi nzima huku kiasi cha chanjo zilizosalia kwenye bohari ya kutunzia chanjo ni 5,266,850 ambazo zote ni aina ya J.J.

Amebainisha kuwa Wizara ya Afya hivi karibuni itazindua ‘Booster’ dozi ya UVIKO-19 ili wananchi waweze kuongeza kinga zaidi dhidi ya ugonjwa huo na kusema kuwa ni hiari kwa mtu yeyote kwenda kupata chanjo hiyo.

Kuhusu huduma za chanjo kwa Watoto, Waziri Ummy amesema huduma hizo ziliendelea kutolewa kwa Watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja kwa chanjo ya Penta3 ambayo hutumika kama kipimo kikuu ilifikia asilimia 107 ukilinganisha na mwaka 2021 iliyofikiwa kwa asilimia 96” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema Wizara imefanikisha vyema Kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio ya matone OPV3 katika raundi zote nne kwa asilimia 103 ukilinganisha na asilimia 79 mwaka 2021, sindano (IPV) kwa asilimia 107 ikilinganishwa na asilimia 95 kwa mwaka 2021, Surua rubella dozi ya kwanza asilimia 109 ikilinganishwa na asilimia 92 kwa mwaka 2021, Surua Rubella dozi ya pili 96% ilinganishwa na asilimia 76 kwa mwaka 2021.