Wizara Ya Afya

AFRIKA YAHIMIZWA KUIMARISHA UWEKEZAJI WA SAYANSI KWA AFYA BORA

Posted on: April 7th, 2026

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), NIMR, na wadau kutoka CHIEB, imezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji katika sayansi, utafiti, na ubunifu. Lengo ni kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora. Wito huu umetolewa  Aprili 7, 2026, jijini dar es salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani.


Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kanda wa WHO Afrika, Dkt.Thomas Fedjo, mtaalamu wa huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage – Life Course) kwa niaba ya mwakilishi mkazi wa WHO Tanzania, amesema Afrika imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya. Mafanikio hayo ni pamoja na maendeleo ya chanjo za Ebola, ugunduzi wa mapema wa aina mpya za UVIKO-19, na juhudi za kuzalisha chanjo barani Afrika.


Amesema changamoto bado zipo,  Afrika inakabiliwa na magonjwa sugu, milipuko mipya, na mifumo dhaifu ya afya. Bw. Fedjo amesema changamoto hizi haziwezi kutatuliwa na nchi moja pekee, bali zinahitaji ushirikiano kati ya serikali, wataalamu, na jamii.

 Mbinu ya “Afya Moja” inasaidia kushughulikia changamoto zinazohusisha binadamu, wanyama, na mazingira.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiufundi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, Shirika la CHIEB Dkt. Siril Kulaya, amesema kuwa uwekezaji katika sayansi na teknolojia za afya ni msingi wa kuhakikisha nchi zinashughulikia milipuko ya magonjwa kwa haraka na kwa ufanisi. Amesisitiza kwamba mradi wa CHIEB unaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kutoa mbinu bunifu za kukabiliana na changamoto za kiafya barani Afrika.


Naye Dkt. Nyanda Elias Ntinginya, Mkurugenzi wa Kukuza na Kuratibu Tafiti, NIMR, ameongeza kuwa NIMR inaendelea kukuza tafiti za kisayansi zinazolenga magonjwa sugu na milipuko mipya. Ameeleza kwamba pamoja na kushirikiana na WHO na CHIEB, NIMR inalenga kuhakikisha matokeo ya utafiti yanatumika kuboresha mifumo ya afya na kunufaisha jamii kwa ujumla.


Nchi 46 za Afrika zimeandaa mipango ya kitaifa ya usalama wa afya, huku kila nchi ikiwa na mkakati wa kukabiliana na usugu wa dawa (Antimicrobial Resistance). Baadhi ya nchi pia zimeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa. WHO inahimiza enzi mpya ya afya barani Afrika inayozingatia huduma kwa wote, mifumo imara, teknolojia za kisasa, na umiliki wa ndani. Hii itasaidia kuhakikisha ubunifu wa Kiafrika unanufaisha jamii nzima.