Wizara Ya Afya

AFRIKA YAASWA KUIMARISHA HUDUMA ZA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA KUPITIA AFYA YA MSINGI

Posted on: June 23rd, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam

Nchi za Afrika zimeshauriwa kuchukua hatua za haraka na za pamoja katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), ambayo sasa yamekuwa tishio kubwa kwa afya, maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii barani humo.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa Kikanda wa PEN-Plus kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza makali (ICPPA 2026), leo Juni 23, 2026, jijini Dar es Salaam

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kisukari, shinikizo la damu, saratani, ugonjwa wa selimundu, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji pamoja na matatizo ya afya ya akili, yanaongezeka kwa kasi na yanahitaji hatua za dharura na ushirikiano wa pamoja.

“Kwa muda mrefu magonjwa hayo yalionekana kuwa ni changamoto ya nchi zilizoendelea, lakini kwa sasa yamekuwa changamoto kubwa kwa nchi za Afrika, yakichangia kuongezeka kwa umaskini wa kaya, kupungua kwa uzalishaji na kuongeza mzigo kwa mifumo ya afya,” amesema Mhe. Mchengerwa

Ameongeza kuwa “Familia zinapokosa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutokana na umbali, gharama kubwa au kutopatikana kabisa kwa huduma, hazipotezi tu fursa ya matibabu, bali pia hupoteza kipato, muda, heshima na wakati mwingine maisha ya wapendwa wao,”

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika huduma za afya ya msingi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kinga, uchunguzi wa mapema, matibabu, ukarabati na ufuatiliaji wa muda mrefu karibu na maeneo wanayoishi.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza husababisha zaidi ya vifo milioni 43 kila mwaka duniani, sawa na asilimia 74 ya vifo vyote. Zaidi ya watu milioni 17 hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka 70, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ikiwemo nyingi za Afrika.