Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YACHOCHEA MABADILIKO YA KIHISTORIA KUPITIA MASHINDANO YA USAFI WA MAZINGIRA

Posted on: April 4th, 2026

Na Happyness Hans, WAF; Dar es Salaam


Wizara ya Afya imeendelea kuendesha mashindano ya afya na usafi wa mazingira kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ambapo mashindano hayo yamekuwa chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya ya mazingira na usafi nchini.


Hayo yameelezwa na Afisa Afya Mazingira Mwandamizi, Nashir Mahiki, leo Aprili 4, 2026, wakati wa zoezi la uhakiki wa mashindano ya afya na usafi wa mazingira kwa mwaka 2026 katika Mkoa wa Dar es Salaam. Zoezi hilo limehusisha halmashauri zote tano za mkoa huo, ambazo ni Ubungo, Ilala, Kigamboni, Kinondoni na Temeke.


Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo, kumekuwa na mafanikio dhahiri katika utekelezaji wa afua za afya ya mazingira na usafi. Miongoni mwa mafanikio hayo ni ongezeko la miji yenye madampo ya kisasa kutoka sifuri mwaka 1988 hadi kufikia madampo nane mwaka 2026, yaliyopo katika jiji la Tanga pamoja na miji ya  Mtwara na Moshi.


Aidha, ameongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la kaya zenye vyoo bora, kutoka asilimia 19.5 hadi kufikia asilimia 78 mwaka 2026. Vilevile, kumekuwepo na uboreshaji wa mazingira ya mijini kupitia bustani za kupendeza pamoja na machinjio yanayokidhi mahitaji ya sasa.


Mahiki ameeleza kuwa, mashindano katika mwaka wa fedha 2025/26 yamehuishwa ili kuongeza uwajibikaji katika utoaji na uimarishaji wa huduma za afya na usafi wa mazingira kwa makundi yanayoshindanishwa.


Amefafanua kuwa, lengo la mashindano hayo ni kuchochea ushiriki wa viongozi, wadau na jamii kwa ujumla katika kuboresha hali ya afya na usafi wa mazingira nchini, pamoja na kuhakikisha usafi wa mazingira, hususani mijini, unakuwa endelevu na wa kudumu.


Katika zoezi hilo la uhakiki, maeneo yaliyopitiwa ni pamoja na udhibiti wa taka ngumu, usimamizi wa maji taka, usafi wa mifereji ya maji ya mvua, usafi wa masoko, upendezeshaji wa miji, usimamizi wa Sheria ya Afya ya Jamii pamoja na sheria ndogo za halmashauri, na usafi wa nyumba za kulala wageni (lodges na hoteli), pamoja na usimamizi wa madampo  ya taka.