WAZIRI MHAGAMA ATEKELEZA MAAGIZO YA MAKAMU WA RAIS UJENZI WA CHUO CHA WAUGUZI
Posted on: January 8th, 2025
Na WAF - Rombo, Kilimanjaro
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametekeleza kwa vitendo maagizo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ya ujenzi wa chuo cha wauguzi kitakachojengwa pembeni ya hospitali ya wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Januari 7, 2024 akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kukagua na kuzindua miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo ya sekta ya afya katika Wilaya ya Rombo pamoja na wilaya ya Same ambapo leo amezindua wodi ya wazazi iliyopo katika kituo cha afya Mkuu - Rombo.
"Ndugu zangu Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haijawahi kupoa, hasa kwenye sekta ya afya, tupo macho kupokea maelekezo na kuyatekeleza, sasa ujenzi wa chuo chetu cha wauguzi utaanza mwezi wa tatu, ili kupunguza tatizo la watumishi ndani ya wilaya, mkoani na Tanzania kwa ujumla," amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema tayari Wizara ya Afya imetenga Shilingi Bilioni Moja ili kuanza haraka iwezekanavyo ujenzi huo ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua vijana zaidi ya 600 na vijana wa bweni wasiopungua 400.
Aidha, Waziri Mhagama amesema ndani ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali yake imetoa Shilingi Bilioni 82 katika wilaya ya Rombo ili kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi katika sekta ya afya ikiwemo ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali.
"Tunaposema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni wa viwango vya juu tunamaanisha kwa sababu miaka iliyopita Rombo haijawahi kupokea fedha nyingi kiasi hiki na hizo Bilioni 82 ni kati ya Bilioni 956 zilizoletwa katika mkoa huu wa Kilimanjaro, hivyo tuna kila sababu ya kumshukuru Rais kwa kuamua kuibeba Tanzania ukiwemo mkoa wa Kilimanjaro kwa kiwango tofauti," amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa mapenzi makubwa ya wananchi wake wa mkoa huo, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu mkoa huo umepokea Shilingi Bilioni 956 za maendeleo.