WAUGUZI, WAKUNGA IMARISHENI MAWASILIANO KATI YENU NA WAGONJWA
Posted on: January 20th, 2025
Na WAF - Pwani
Wauguzi na wakunga wametakiwa kuimarisha mawasiliano bora na wagonjwa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya, kuanzia huduma za afya ngazi ya msingi.
Hayo yamesemwa Januari, 18 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Bw. Paul Magesa, wakati akihitimisha kikao kazi cha kupitia na kuhakiki kitita cha huduma staha zinazozingatia utu, heshima, na maadili.
“Vipaumbele vya Wizara ya Afya ni kuhakikisha ubora wa huduma kwa wananchi, ambapo mawasiliano na lugha ya staha ni sehemu muhimu ya malengo haya. Mawasiliano ya staha ni sehemu ya miongozo ya maadili kwa wauguzi na wakunga, kwani yanachangia katika kujenga uaminifu na kuboresha uhusiano na wagonjwa, ”amesema Bw. Magesa.
Bw. Magesa amesema wauguzi na wakunga wanachangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma za afya, wakiwa ni asilimia 60 ya watoa huduma katika sekta hii. Kwakuwa wao ndio wanaotangamana zaidi na wagonjwa kila siku, mchango wao ni muhimu sana katika kuboresha hali ya afya ya jamii.
“Ili kuboresha mawasiliano kati ya wauguzi na wagonjwa, ni muhimu kuweka nyenzo zinazowawezesha wauguzi kuwahudumia wagonjwa,” amesema Bw. Magesa.
Hiki kitita kinajikita katika miongozo ya maadili kwa wauguzi na wakunga kazini, ambapo mawasiliano bora na uwazi ni muhimu katika kuboresha huduma za afya.