WATAALAM WA OPTOMETRIA ZINGATIENI MAWANDA YA MAJUKUMU YENU
Posted on: January 16th, 2025
Na WAF, Dodoma
Wanataaluma ya optometria nchini wametakiwa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia mawanda ya majukumu yao pamoja na sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya taaluma zao.
Hayo yamesemwa Januari 16, 2025 na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya Bi. Grace Sheshua wakati wa mafunzo ya maadili na hafla ya utoaji vyeti kwa wataalam wa kada ya optometria ngazi ya shahada na stashahada waliopata usajili wa kudumu na usajili wa awali, Jijini Dodoma.
Bi. Sheshua amehimiza Mabaraza ya kitaaluma kuhakikisha wataalam hao wanaowasimamia wanatoa huduma kwa kufuata miongozo hiyo na kufatilia mienendo yao wakiwa mahala pa kazi.
“Baadhi ya wataalam wamekuwa wakitekeleza majukumu yasiyo ya kwao na kusababisha changamoto mbalimbali za uoni kwa jamii, hivyo ni vyema kufanya kazi ile unapaswa kuifanya pekee,” amesema Bi. Sheshua
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuweka juhudi kubwa katika huduma za macho kwa kuhakikisha kuwa inatekeleza mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya ya Macho wa 2022- 2027 lengo likiwa ni kupunguza upofu na ulemavu wa macho miongoni mwa Watanzania.
“Wizara ya Afya kupitia mpango wa Taifa wa Huduma ya Macho imejitahidi kuhakikisha kuwa, kila hospitali ya mkoa na hospitali nyingi za wilaya zinakuwa na idara ya macho inayotoa huduma ya kina ya macho ikiwa ni pamoja na huduma za optometria,” amesema Bi. Sheshua.
Awali akimkaribisha Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu, Mwenyekiti wa Baraza la Optometria Tanzania Dkt. Anna Sanyiwa amewataka wataalam hao kuipenda na kuionea fahari taaluma yao na kwenda kutoa huduma bora za macho kwa Watanzania pamoja na kujikita katika bunifu mbalimbali za fani hiyo ili kuzidi kuikuza taaluma hiyo.
Naye Msajili wa Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Milanzi ametoa rai kwa wataalam hao kuyazingatia yale yote waliyofundishwa wakati wa mafunzo hayo na kuonya juu ya ukiukwaji wa sheria, kanuni na miiko ya kitaaluma na kusema kuwa Baraza litachukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kusitisha au kufuta usajili endapo ukiukwaji huo utajitokeza kwa yeyote yule.