Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGONJWA 26 WAMEPANDIKIZWA FIGO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Posted on: February 14th, 2022

Hospitali ya Benjamin  Mkapa imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 26 kuanzia machi 22, 2018 kutoka mikoa mbalimbali nchini na wote wanaendelea vizuri.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa idara ya Magonjwa ya Figo Dkt. Anthony Gyunda kwenye kipindi cha Mirindimo kinachorushwa na TBC Taifa.

"Uharibifu wa Figo unasababishwa na taka sumu pamoja na magonjwa yote yanayoathiri mwili kama kisukari, shinikizo la damu na presha pamoja na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza." amesema Dkt. Gyunda

"Kuna hatua tano za matibabu ukigundulika na ugonjwa wa Figo ikiwepo hatua ya haraka ambayo ni uchujaji wa damu na hatua ya mwisho ni upandikizaji wa figo."amesema Dkt. Gyunda 

Aidha, Dkt. Gyunda ametoa ushauri kwa wananchi kuepuka matumizi ya ulaji wa nyama kwa wingi, utumiaji wa sukari, mafuta ya kula pamoja na unywaji wa pombe ili kuepuka Magonjwa yasiyokuwa ya lazima ikiwemo ugonjwa wa figo.

"Epukeni matumizi holela ya dawa, nendeni mkapate vipimo na ushauri wa wataalamu kwakuwa matumizi ya Dawa kiholela sio mazuri kiafya na hii hupelekea kuua mfumo wa Figo."amesema Dkt. Gyunda 

Hivyo basi, Dkt. Gyunda amewasihi wananchi kupata vipimo kila mara, angalau mara mbili kwa mwaka ili kujua Afya zao na kuepuka gharama za matibabu.

Dkt. Gyunda amesema katika hospitali hiyo wanapokea wagonjwa mbalimbali kutoka Mikoa jirani ikiwemo Iringa, Singida, Manyara na Mikoa mengine.

Pia ameishukuru Serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuwawezesha upatikanaji wa watumishi wenye weledi pamoja na vifaa tiba.

Mmoja wa wagonjwa katika kitengo cha Figo ambaye ni kijana mwenye mwenye umri wa miaka 17 amesema anapata matibabu ya uchujaji wa Damu katika hospitali hiyo na anaendelea vizuri. 

Kwa upande wake mtaalamu wa Magonjwa ya uti wa mgongo Dkt. Waziri Jimmy amesema sio lazima kila tatizo kufanyiwa upasuaji Magonjwa mengine yanaisha kwa kutumia dawa. 

"Ili kujua tatizo mapema lazima kupata vipimo kwa kuwaona Wataalamu kabla ugonjwa haujazidi hadi kupelekea kufanyiwa upasuaji." amesema Dkt. Jimmy 

Mara nyingi magonjwa yasiyoambukiza hayana dalili hivyo ni muhimu kujua Afya yako kabla ya tatizo kujitokeza, afadhali kutumia gharama za vipimo kuliko kutumia gharama za matibabu.