TUNDUMA YAONGEZA UTAYARI WA KUKABILIANA NA TISHIO LA EBOLA MIPAKANI
Posted on: July 11th, 2026Na Happyness Hans, WAF - Tunduma
Kituo cha Afya cha Mpakani Tunduma mkoa wa Songwe kimeendelea kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kufuatia ziara ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya waliotembelea kituo hicho kwa lengo la kukagua kiwango cha utayari na mifumo ya kudhibiti ugonjwa huo endapo utatokea.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, leo Julai 11, 2026 Afisa Afya wa Mpaka wa Tunduma, Bw. Paul Mafuru, amesema ujio wa wataalamu hao unadhihirisha dhamira ya Wizara ya Afya ya kuhakikisha vituo vya mipakani vinakuwa tayari kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan Ebola. Amesema ukaguzi huo umejikita katika tathmini ya mifumo ya uchunguzi wa wasafiri, maeneo ya kutenga wahisiwa pamoja na hatua zinazochukuliwa baada ya kubainika kwa mgonjwa mhisiwa.
Amesema kituo hicho kina uwezo wa kutambua wahisiwa wa Ebola kupitia utaratibu wa uchunguzi (screening) unaofanyika kwa wasafiri wanaoingia nchini.Aidha, amesema kuna eneo maalumu la kutenga wahisiwa (Isolation Room) lenye mazingira salama wakati taratibu za kuwahamishia kwenye vituo vya matibabu zinapoendelea.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi wa Huduma za Dharura na Ajali kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bw. Kanisius Nyakaselula, amesema eneo la kutenga wahisiwa limeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Amefafanua kuwa eneo hilo lina wahudumu wa kiume na wa kike, vyoo, milango inayokidhi viwango vya usalama pamoja na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kuwahudumia wahisiwa.
Ameongeza kuwa huduma za usafirishaji wa wahisiwa zimeimarishwa kupitia gari la wagonjwa (ambulance) lililo tayari wakati wote kwa ajili ya kumhamisha mgonjwa muhisiwa kwenda Kituo cha Matibabu ya Ebola (ETC) kilichopo Chipaka kwa uchunguzi na matibabu zaidi endapo itahitajika.
Maandalizi hayo yanaonyesha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi dhidi ya magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya mipakani, hususan kutokana na uwepo wa milipuko katika baadhi ya nchi jirani.