TIBA BORA YA MOYO NCHINI NI MATOKEO YA UWEKEZAJI THABITI WA SERIKALI AWAMU YA SITA
Posted on: July 10th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF - Dar-es-Salaam
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu, kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge amesema hayo leo Julai 10, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo la tiba ya Michezo kwaajili ya maandalizi ya AFCON 2027 inayofanyika Hospitali ya Dar Group jijini Dar-es-salaam.
"Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, JKCI imepiga hatua kubwa kwa kupanua huduma zake kupitia kuanzisha matawi katika maeneo mbalimbali nchini, hatua iliyochochea upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi na kupunguza ulazima wa kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu Dar es Salaam," amesema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge amesema, michezo ni sehemu muhimu ya kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, hususan magonjwa ya moyo, ambapo amesema kuwa kutembea ni aina ya mazoezi yanayochangia kuboresha afya na kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
"Ujenzi wa Kituo cha Tiba ya Michezo utaimarisha juhudi hizi kwa kuwahudumia wanamichezo na wananchi kwa ujumla ndani na nje ya nchi.” amesema Dkt. Kisenge
Aidha, amesema JKCI imeendelea kuimarisha uwezo wa utoaji huduma kwa kuongeza wataalamu, kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa watumishi, kuboresha vifaa tiba vya kisasa ikiwemo vinavyotumia teknolojia ya akili mnemba (Artificial Intelligence), pamoja na maabara za kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo (Cath Lab), hatua zinazoiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma kwa viwango vya kimataifa.
“Kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, JKCI imeendelea kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kwa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali nchini, Dhamira yetu ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za moyo kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi.” amesema Dkt. Kisenge.