Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA, KOREA WAZINDUA MRADI WA USHIRIKIANO WA UBORESHAJI MAABARA YA TAIFA YA AFYA YA JAMII

Posted on: June 19th, 2025

Na WAF, Dar es Salaam


Serikali za Tanzania na Korea zimezindua Mradi wa Ushirikiano kati ya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL) na Taasisi ya KOFIH ya Korea utaiwezesha  NPHL kufanya kazi kwa ufanisi zaidi


Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura Dkt. Erasto Sylvanus ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya amebainisha hayo katika hafla ya uzinduzi wa mradi  wa ushirikiano wa Taasisi hizo mbili leo Juni 19, 2025  iliyofanyika katika ofisi ya Maabara ya Taifa iliyopo kwenye ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Jijini Dar es Salaam.


Ili kutekeleza mradi huo kwa ufanisi  Dkt. Sylvanus amesema Taasisi ya KOFIH itatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kwa miaka mitano, ambapo kwa sasa imetoa kiasi cha Bilioni 1.1 zitakazotumika kufanya utafiti wa vijidudu vinavyosababisha  magonjwa kama vile Dengue, chikungunya na magonjwa ya njia ya hewa pamoja na utaalam wa kupima sampuli na kutambua magonjwa kwa haraka zaidi.


"Mradi huu utasaidia kugundua magonjwa kwa wakati tofauti na kama ilivyokuwa awali kwani imekuwa ni kawaida mwananchi anapohisi kuwa na malaria hupima na vipimo vinapoonesha kuwa hana ugonjwa huo

 huridhika kuwa yuko salama, lakini kwa sasa vipimo hivyo havitaishia hapo bali vitaenda mbali zaidi kuchunguza magonjwa mengine," amefafanua Dkt. Sylvanus.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa -NPHL Bw.  Ambele Mwafulango amesema Taasisi ina uwezo wa kupima sampuli mbalimbali na kutoa  majibu ya uhakika kwani ina ithibati ya umahiri na kutambulika kimataifa.


Amesema mradi huo unaozinduliwa leo utawawezesha kuboresha zaidi utendaji kazi kwa kutoishia kupima sampuli pekee bali pia kutafuta chanzo cha uwepo wa vijidudu hivyo  na jinsi ya kukabiliana navyo kupitia tafiti zitakazofanywa.


Naye  Mtaalam wa Afya wa Taasisi  ya KOFIH Bw. Hansol  Park amesema Taasisi yake itahakikisha kuwa ushirikiano huo unakuwa ni wenye manufaa kwa kuhakikisha kuwa wataalam wanapatiwa mafunzo  zaidi.