SONGWE YAISHUKURU WIZARA YA AFYA KWA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA MAGONJWA YA MLIPUKO
Posted on: July 9th, 2026Na. Happyness Hans, WAF - Songwe
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Agustino Simon, amesema Mkoa huo unaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuusaidia katika kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya dharura na maafa kupitia mafunzo na usimamizi shirikishi, hususan katika kipindi hiki cha tahadhari ya ugonjwa wa Ebola pia
zimesogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuongeza uwezo wa wataalamu wa afya.
Amesema hayo leo Julai 9, 2026 mkoani Songwe, Dkt. Simon amesema Mkoa wa Songwe, unaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya mipakani ili kuzuia magonjwa hayo kuingia nchini.
Amebainisha kuwa hadi sasa mkoa huo haujaripoti kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola kutokana na hatua mbalimbali za kinga zinazoendelea kutekelezwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Songwe, Dkt. Wilson Albert, amesema ziara ya timu ya Wizara ya Afya imewajengea uwezo wataalamu wa hospitali hiyo na kuchangia kuboresha utoaji wa huduma. Amesema maboresho hayo yamerahisisha wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao na kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za Rufaa na Taifa.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Wagonjwa Mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe, Dkt. Issa Kisoma, ameishukuru timu ya usimamizi shirikishi kutoka Wizara ya Afya kwa kutoa mafunzo yaliyowasaidia kubaini maeneo ya kuboresha huduma na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za afya.
Aidha, ameishukuru Wizara kwa kuendelea kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba na kupongeza watumishi kwa kuzingatia usafi pamoja na matumizi sahihi ya vifaa hivyo.
Hatua hizo zinaendelea kuimarisha utayari wa Mkoa wa Songwe katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wakati.