SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 18 KUIMARISHA HUDUMA ZA MOYO, KUKUZA TIBA YA MICHEZO NA TIBA UTALII
Posted on: July 10th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF – Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza takribani Shilingi bilioni 18 katika ujenzi wa Kituo cha Tiba ya Michezo, hatua inayolenga kuimarisha huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya moyo, kuongeza ubora wa huduma za afya na kukuza tiba utalii nchini.
Uwekezaji huo pia unatarajiwa kuboresha utambuzi wa magonjwa ya moyo kwa haraka na kwa usahihi, huku ukiimarisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kuwa kitovu cha huduma za moyo kinachotambulika katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Hayo yamebainishwa leo Julai 10, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Tiba ya Michezo kwa ajili ya maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), iliyofanyika katika Hospitali ya Dar Group jijini Dar es Salaam.
"Uwekezaji huu ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya kwa wanamichezo na wananchi kwa ujumla. Kituo hiki kitakapokamilika na kitatoa huduma za uchunguzi, ushauri wa kitaalamu na matibabu kwa viwango vya kisasa," amesema Dkt. Samizi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za kinga na elimu ya afya kupitia JKCI Health Promotion Studio kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na kuhamasisha jamii kuzingatia kinga kabla ya tiba.
Dkt. Samizi ametumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini mapema viashiria vya magonjwa na kupata matibabu stahiki kabla hayajaleta madhara makubwa.
"Natoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara, kwa sababu ugunduzi wa mapema wa viashiria vya magonjwa huwezesha kupata tiba stahiki na kuepuka madhara makubwa yanayotokana na magonjwa," amesisitiza Dkt. Samizi.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kupitia ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, hospitali za rufaa, huduma