Wizara Ya Afya

SERIKALI YAIMARISHA UWEZO WA WAHUDUMU HOSPITALI YA MJI TUNDUMA KATIKA HUDUMA ZA DHARURA, AJALI NA MAHUTUTI

Posted on: July 11th, 2026

Na Happyness Hans, WAF-Tunduma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha uwezo wa utoaji wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi (ICU) kufuatia ziara ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya iliyofika hospitalini hapo kwa lengo la kutathmini kiwango cha utayari wa huduma, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na kuboresha matumizi ya vifaa tiba vinavyotumika katika kuhudumia wagonjwa.

Akizungumza leo Julai 11, 2026 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Tunduma, Dkt. Peter Mapunda, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa hospitali hiyo kutokana na kuwapa wahudumu nafasi ya kujifunza mbinu za kisasa za utoaji wa huduma za dharura, ikiwemo namna sahihi ya kuwahudumia wagonjwa pamoja na matumizi bora ya mashine na vifaa tiba vinavyotumika katika kuokoa maisha.

Dkt. Mapunda ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, watumishi wa hospitali wamepata uelewa mpya na kuongezewa uwezo wa kitaalamu, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura. Amebainisha kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Afya na wahudumu wa hospitali umeendelea kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Aidha, ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya kupitia upatikanaji wa vifaa tiba na mashine mbalimbali zinazowezesha utoaji wa huduma za dharura kwa ufanisi zaidi. Pia amepongeza timu ya Wizara ya Afya kwa kutoa mafunzo yenye tija na kushirikiana kwa karibu na watumishi wa hospitali katika kuboresha huduma.

Kwa upande wake, Muuguzi wa Hospitali ya Mji Tunduma, Bi. Sophia Mwanja, amesema ujio wa wataalamu kutoka Wizara ya Afya umeongeza maarifa na ujuzi wa wahudumu wa kitengo cha dharura. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamejikita katika mbinu mbalimbali za utoaji wa huduma na matumizi sahihi ya vifaa tiba, hali inayotarajiwa kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.