Wizara Ya Afya

SERIKALI YAIMARISHA MIFUMO YA MAPATO SEKTA YA AFYA

Posted on: March 27th, 2026

Serikali imejipanga kuimarisha ukusanyaji wa mapato na matumizi ya bajeti katika Sekta ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza leo Machi 26, 2026, jijini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara imeendelea kuimarisha mifumo ya mapato sambamba na usimamizi wa matumizi ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa tija.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara na taasisi zake zilikadiria kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 819.9, ambapo hadi kufikia Februari 2026 jumla ya shilingi bilioni 494.6 zimekusanywa sawa na asilimia 60.33 ya lengo.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Wizara iliidhinishiwa zaidi ya shilingi trilioni 1.76 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo, ambapo hadi Februari 2026 kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 1.0 kimepokelewa sawa na asilimia 57 ya bajeti iliyoidhinishwa.

Amebainisha kuwa, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali itaendelea kuimarisha vyanzo vya mapato, kuongeza ufanisi wa mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na kupanua wigo wa huduma za bima ya afya kwa wote.

“Lengo letu ni kuhakikisha Sekta ya Afya inakuwa na rasilimali za kutosha ili kuboresha utoaji wa huduma kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuongeza wataalam wa kada mbalimbali pamoja na kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba ili kukidhi mahitaji ya wananchi.