Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA MIPAKANI KUDHIBITI MAGONJWA YA MILIPUKO

Posted on: July 12th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Rukwa

Serikali imeendelea kuimarisha huduma za dharura katika maeneo ya mipakani ili kuongeza utayari wa kugundua mapema, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kuvuka mipakani

Hayo yamesemwa leo Julai 12, 2026 na Dkt. Michael Kiremeji, Daktari Bingwa wa Huduma za Dharura kutoka Wizara ya afya, wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi wa utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika Kituo cha Mpakani cha Kasesya, mkoani Rukwa.

Amesema lengo la zoezi hilo ni kutathmini utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya, kubaini maeneo yenye changamoto na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya kuboresha huduma.

Amesema vituo vya mipakani vina jukumu muhimu katika kuzuia kuingia na kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko, hivyo ni muhimu kuhakikisha mifumo ya uchunguzi wa wasafiri, utoaji wa huduma za dharura na uratibu wa taarifa za afya unaendelea kuimarishwa wakati wote.

Aidha, Dkt. Kiremeji amesema Wizara ya Afya itaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu katika maeneo ya mipakani ili kuhakikisha viwango vya utayari vinaendelea kuongezeka na watumishi wa afya wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa ya afya ya umma.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Huduma za Afya Mipakani katika Kituo cha Mpakani cha Kasesya, Yustus Landula, amesema zoezi hilo limekuwa fursa muhimu ya kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuimarisha ushirikiano kati ya watumishi wa afya na taasisi nyingine zinazofanya kazi mpakani.

Ameeleza kuwa wataendelea kutekeleza maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha Kituo cha Mpakani cha Kasenyi kinaendelea kuwa imara katika kulinda afya ya wananchi na wasafiri wanaotumia mpaka huo.