Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUGAWA VYANDARUA ZAIDI YA MILIONI 1.5 SHINYANGA

Posted on: January 8th, 2025

Na WAF, SHINYANGA

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI, wameanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa kila kaya,ili kupambana na ugonjwa wa malaria mkoani Shinyanga, mkoa wenye maambukizi ya asilimia 16 kwa sasa.

Hayo yamesemwa Januari 6, 2025 na Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Bw. Peter Gitanya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria (NMCP), kwenye kikao kazi na waandishi wa habari 25 wa Klabu ya Waandishi mkoani hapa.

Amesema Serikali kupitia mpango wake wa kudhibiti malaria nchini, imeanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa wananchi kwa kila kaya, ili kupambana na ugonjwa wa malaria na kuutokomeza ifikapo 2030.

“Mkoa wa Shinyanga vitasambazwa vyandarua vyenye dawa milioni 1.5 na kaya zote zitafikiwa na sasa tupo kwenye zoezi la uandikishaji kaya kwa kaya, na chandarua kimoja watapewa watu wawili kwa kila kaya,”amesema Bw. Gitanya.

Kuhusu Kaya ambayo haitaandikishwa haitapatiwa chandarua, na kuwasihi washiriki zoezi hilo kikamilifu, ambapo maafisa watakuwa wakipita kwenye kaya zao kuchukua taarifa pamoja na kuwapatia kadi maalumu kwa ajili ya kuja kupewa chandarua.

Amongeza kwamba zoezi la uandikishaji lilishaanza tangu Januari 2, 2025 na litakwenda hadi Januari 15, na tarehe 16 zoezi rasmi la usambazaji vyandarua litaanza na kuzifikia kaya zote ambazo zimeandikishwa.

Aidha, akizungumzia hali ya malaria nchini, ameutaja mkoa wa Shinyanga kwamba unashika nafasi ya nne (4) kitaifa, kuwa na kiwango cha juu cha malaria asilimia 16, huku Tabora ikishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 24, Mtwara asilimia 20, na ya tatu (3) ni Kagera asilimia 18.ambapo maambukizi kitaifa ni asilimia 8 tu.

Naye Bi. Happines Nania kutoka Wizara ya Afya, amesema kwa mwananchi ambaye atapoteza kadi ambayo atapewa wakati akiandikishwa kwa ajili ya kupewa chandarua, antapaswa kwenda kwenye kituo husika ili kupewa chandarua chake sababu taarifa zake zitakuwepo,huku akisisitiza pia utunzaji wa vyandarua hivyo na kuvitumia kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa.