Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MTOTO MCHANGA WA SIKU 15 ALIYEZALIWA NA VIUNGO VYA ZIADA AFANYIWA UPASUAJI WA KIPEKEE MBEYA

Posted on: June 21st, 2025

Na WAF Mbeya, 


Timu ya Madaktari Bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo  Juni 20, 2025 wamefanya upasuaji wa kipekee kwa mtoto mchanga mwenye umri wa siku 15  aliyezalizwa na baadhi ya viungo vya ziada. 



Viungo hivyo kwa kitaalam polymelia  viliunganika katika sehemu ya mgongo ya mtoto huyo ukiwemo mguu wa ziada, sehemu ya siri, na sehemu ya utumbo uliojitenga . 


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya upasuaji huo, Kiongozi wa timu hiyo Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji wa Watoto Dkt. Lazaro Mboma, amesema viungo hivyo vya ziada vinaweza kusababisha changamoto kubwa katika utendaji kazi wa mwili, ikiwa ni pamoja na ugumu wa kutembea, kufanya kazi za kila siku,  maumivu na kuathiri ubora wa maisha yake.


Dkt. Mboma alitaja athari nyingine kuwa  inaweza kusababisha sintofahaumu katika kijamii iliwemo pia changamoto ya  kisaikolojia kwa mtoto na familia yake.


“Upasuaji huu ni mchakato mgumu ambao unahitaji ujuzi wa hali ya juu na umakini mkubwa uliotumia takribani  saa moja na dakika kumi na umefanyika kwa mafanikio makubwa bila kuathiri afya ya viungo vingine na hali ya mtoto huyu inaendelea vizuri," amesema Dkt. Mboma.


Ameeleza kuwa upasuaji huo  ni hatua kubwa kwa huduma za afya za mkoa wa Mbeya, na wataendelea kutoa huduma zaidi za kibingwa bobezi kwa watoto na wagonjwa wengine.


Wakati huohuo, familia ya mtoto aliyefanyiwa upasuaji imeelezea furaha yao na kuishukuru  timu ya madaktari na watoa huduma wote hospitalini hapo  kwa jitihada zao za kuhakikisha mtoto wao anapatiwa matibabu bora na salama.


“natoa shukrani zetu za dhati kwa timu ya madaktari na wauguzi kwa msaada wao katika matibabu ya mwanangu. Kwa sasa mtoto wetu anaendelea na matibabu na afya yake inaendelea kuimarika”  amesema  Bi. Lina Kasanya ambaye ni mama wa mtoto huyo.