MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA MOI YAIMARISHA HUDUMA ZA UBINGWA, UBINGWA BOBEZI
Posted on: March 6th, 2025
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma zake, hususan kwa kupanua wigo wa huduma za kibobezi zikiwemo uchunguzi na upasuaji wa ubongo, nyonga na magoti, pamoja na upasuaji wa migongo kwa njia ya kufungua.
Hayo yameelezwa Machi 5, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Mpoki Ulisubisya, wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Mpoki amesema kumekuwa na uwekezaji mkubwa katika mafunzo na utafiti, hali ambayo imechangia ongezeko la wataalam waliobobea katika sekta ya mifupa na mishipa ya fahamu na kwamba hatua hiyo imeongeza ufanisi wa matibabu yanayotolewa kwa wagonjwa.
Amesema katika kipindi cha miaka minne, MOI imehudumia jumla ya wagonjwa 816,400, huku zaidi ya wagonjwa 7,000 wakinufaika moja kwa moja na huduma za kibobezi.
"Serikali kupitia Taasisi ya MOI, imewezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupimia wagonjwa, hatua ambayo imeongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa mahututi," amesema Dkt. Ulisubisya.
Aidha, Taasisi imepokea mradi wa kufua hewa oksijeni wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.7 ambao unatarajiwa kuokoa Shilingi Milioni 1.2 zilizokuwa zikitumika kununua oksijeni hiyo kila mwaka.
Ameongeza kuwa MOI pia imefanikiwa kutekeleza mpango wa “Tiba Mkoba,” ambao umelenga kuwafikia wananchi walioko maeneo ya mbali na kuwapatia huduma za kibobezi. Kupitia mpango huo, jumla ya wagonjwa 4,496 wamepatiwa huduma za kibingwa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Aidha Dkt. Ulisibisya amesema, MOI inaendelea kusimamia ujenzi wa hospitali ya utengamao kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kurejesha afya zao baada ya upasuaji au ajali.
Ameongeza kuwa ujenzi huo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na huduma za afya zinazolingana na viwango vya hospitali kubwa duniani, hivyo kupunguza utegemezi wa rufaa za matibabu nje ya nchi.