Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA, AJALI NA AFYA YA AKILI YANAZUILIKA

Posted on: November 10th, 2022

Na. WAF - Mwanza 


Imeelezwa kuwa mbinu muhimu za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na kubadili mtindo wa maisha kwa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe, matumizi ya sukari na chumvi, kufanya mazoezi ya mwili pamoja na kuepuka tabia bwete.


Akifungua Kongamano la nne la Kisayansi katika wiki ya maadhimisho ya wiki ya Magonjwa Yasiuoambukiza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na kununua vifaa tiba vya kisasa vikiwemo vifaa vya uchunguzi  vinavyowezesha wanasayansi kufanya kazi zao kiurahisi ili kugundua magonjwa mapema hususan yasiyoambukiza. 


"Kwa sasa tumeshuhudia maboresho yaliyofanyika katika taasisi zetu za Ocean Road, NIMR, JKCI, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Kanda, Hospitali za Mikoa, Wilaya hadi Zahanati pamoja na Hospitali binafsi." Amesema Prof. Mdoe


Huduma za Uchunguzi na utambuzi wa magonjwa (Maabara), Mionzi na Radiolojia zimeboreshwa kwa maana ya miundombinu na vifaa vya kisasa ili kurahisisha utoaji huduma ya magonjwa yasiyoambukiza na uwezo wa kufanya tafiti mbambali za kisayansi.


Aidha, Prof. Mdoe ametoa wito kwa taasisi kujiwekeza katika kutoa huduma, waongeze kasi pia ya kufanya tafiti za kisayansi zitakazowezesha wananchi kujikinga na magonjwa haya na pia zitakazowezesha kutoa mbinu mpya za matibabu


Pia, amewataka wataalamu hao kujadiliana juu ya matumizi ya dawa za asili ambazo nyingine zimekuwa zikitumika kutibu pumu, shinikizo la juu la damu na Saratani.


"Tuweke mfumo sahihi wa kuwezesha dawa hizi za asili zikithibitika kisayansi kuwa zinatibu na hazina madhara ili tuweze kuzitumia kudhibiti magonjwa haya yasiyoambukiza." Amesema Prof. Mdoe 


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya kazi na wadau wote wenye nia ya kusaidia mapambano dhidi ya magonjwa Yasiyoambukiza, kwani bila kufanya hivyo mlipuko wa magonjwa haya utaendelea kuua watu wengi, kuleta ulemavu na mwisho kurudisha nyuma jitihada za Taifa kukuza uchumi. 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Tiba Prof. Paschal Ruggajo amempongeza Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulipa kipaumbele swala la mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na sasa ameipa kazi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi, kifua kikuu kusimamia maswala ya Magonjwa Yasiyoambukiza. 


"Tunatambua mchango mkubwa wa Bunge katika  kuimarisha afya za watanzania." Amesema Prof. Ruggajo 


Wizara ya Afya kupitia Idara ya Huduma za Tiba inaratibu kitengo na Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, inatekeleza afua mbalimbali ili kuongeza nguvu na kuweza kufikia malengo ya kuzuia na kudhibiti Magonjwa hayo.


"Hii kauli mbiu ya mwaka huu ya Badili Mtindo wa Maisha, Boresha Afya lengo lake kuu ni kuitaka jamii ya watanzania na wadau wote kushirikiana katika kubadili mtindo wa maisha ili kuwa na afya bora na yenye kuleta tija kwa Taifa letu." Amesema Prof. Ruggajo


#MtuNiAfya 

#JaliAfyaYako