Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WATUA TANGA KUTOA HUDUMA KATIKA HOSPITALI ZA WILAYA 11

Posted on: May 20th, 2024



Na WAF – Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka Madaktari bingwa wa Rais Samia kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, weledi na utu katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafundisha wataalamu watakaofanya nao kazi katika vituo walivyopangiwa

Dkt. Batilda ameyasema hayo mapema leo Mei 20, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga katika uzinduzi wa Kambi za Matibabu ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia katika ngazi ya Wilaya ambapo Madaktari hao watatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa katika Hospitali zote 11 za Wilaya zilizo Mkoani Tanga.

Bi. Batrida ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuijali Sekta ya Afya nchini katika kuanzisha huduma mbalimbali zikiwemo za kibingwa na ubingwa bobezi ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, uboreshaji wa miundombinu pamoja na huduma za vipimo ikiwemo kipimo cha CT scan ambayo inapatikana katika Hospitali za Rufaa za Mikoa yote nchini.

Kwa Upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuruhusu huduma hizi kufanyika kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwataka wataalam wa Hospitali hizo kuchukua ujuzi wa Madakatri Bingwa wanaoenda katika vituo vyao.

“Naishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu huduma mkoba hizi kuendelea katika Halmashauri zote 184 chini, tulianza na Kambi za Matibabu ya Madaktari Bingwa Ngazi ya Mkoa na sasa rasmi tumehamia kwenye Hospitali za Wilaya, na kote tulikopita wananchi wamepongeza kambi hizi kwa kuwa msaada kwao juu ya changamoto mbalimbali za kiafya zilizokuwa zikiwakabili”. Amesema Mhe. Ummy.

Waziri Ummy ameongeza kuwa baada ya kambi hizi kuanzishwa zimewasaidia wengi kuondokana na changamoto za kiafya walizokua nazo ambapo tangu zoezi lilipozinduliwa rasmi tarehe 6 Mei 2024 zaidi ya watu 20,000 wameonwa na wamepata matibabu makubwa.