MADAKTARI BINGWA WA DKT. SAMIA WAHUDUMIA ZAIDI YA WANANCHI 2000 TEMEKE
Posted on: January 20th, 2025
Na WAF, TEMEKE
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro amesema wananchi zaidi ya 2000 wamefanikiwa kupata huduma ya matibabu ya kibingwa kweye kambi ya Siku tano iliyowekwa Hospitalini hapo.
"Wakati wa kambi hii maalumu wananchi wapatao 2442 tumewapatia huduma za matibabu kikamilifu ambapo kati yao wanawake ni 1,478 sawa na asilimia 61 ya wagonjwa wote waliohudumiwa na wanaume idadi yao ikiwa ni 964 sawa na asilimia 39 ya wagonjwa waliohudumiwa huku watoto chini ya miaka mitano waliohudumiwa ni 282," amesema Dkt. Kimaro.
Dkt. Kimaro amesema katika utoaji wa huduma kwenye Kambi hiyo maalum imebainika kuwa wagonjwa wengi waliohudumiwa ni wale wenye magonjwa yasiyoambukiza ambapo idadi ya wagonjwa wenye magonjwa hayo walikuwa 1538 ikiwa ni sawa na asilimia 63 ya wagonjwa wote waliohudumiwa.
"Madaktari hao Bingwa 55 wa magonjwa mbalimbali walifanikiwa kutoa huduma za kibingwa ikiwepo upasuaji kwa wagonjwa 59.
Wakati wa zoezi hilo, upande wa maabara ilifanikiwa kufanya vipimo 1861 kwa ufanisi mkubwa na huduma za radiolojia vilikuwa vipimo 702 ikiwemo vipimo vya Ultrasound, CT Scan na X-ray," amengeza Dkt. Kimaro.
Kwa upande wake Dkt. Bryceson Kiwelu aliyekuwa miongoni mwa Madaktari Bingwa amesema, kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa kuwa ni wanawake na wenye magonjwa ya kuambukiza ameshauri jamii kuendelea kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kuepukana na maradhi hayo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Deus Buma ameishukuru Serikali kupitia wizara ya Afya na ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam kwa kukamilisha zoezi hilo muhimu la kambi kwani inawezesha wananchi wanapata matibabu kwa gharama nafuu.