Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KIPIMO CHA MRI SASA KUPATIKANA NKINGA

Posted on: December 21st, 2024


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi mashine ya MRI inayotoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na majeraha makubwa ya mifupa na ubongo katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, inayomilikiwa na kanisa la 'Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT).

Waziri Mhagama amezindua huduma hiyo leo Desemba 20, 2024 Mkoani Tabora, itakayowasaidia Watanzania wote hususani wanaoishi Kanda za Magharibi pamoja na kanda ya Ziwa.

"Tumezindua rasmi huduma za kipimo cha mashine ya MRI ambacho ni kipimo cha kibobezi kinachotoa huduma ya mionzi na sumaku kwa uchunguzi wa wagonjwa kwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na waliopata majeraha makubwa ya mifupa na ubongo," amesema Waziri Mhagama.

Amesema, kipimo hicho kinawasadia madaktari kutoa matibabu sahihi na kwa wakati hivyo kuzuia madhara makubwa ambayo yangeweza kujitokeza ikiwemo kifo.

Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma hizi za kipimo cha MRI zinaingizwa katika utaratibu wa matibabu ya Bima ya Afya ya Taifa ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hizo kwa urahisi bila kikwazo cha fedha.

"Serikali kupitia Wizara imeanzisha utaratibu wa kuzipeleka huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi ambapo kambi za madaktari bingwa zijukanazo kama "Madaktari bigwa wa Dkt. Samia" ambao walitoa huduma katika halmashauri zote 184 kwa fani Sita (6) yakiwemo magonjwa ya ndani, magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto, upasuaji, kinywa na meno na mifupa," amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama ametoa wito kwa Watanzania wote kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora na kuwahamasisha kufika kwenye vituo vya afya pindi wanaposikia mabadiliko yoyote ya kiafya ili kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu sahihi na kwa wakati.

Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga Dkt. Titto Chaula amesema kuwa Hospitali hiyo ina madaktari bingwa 13 wakiwemo wabobezi wawili wa moyo pamoja na mifupa, lengo likiwa ni kusogeza huduma hizo karibu na wananchi ili wasipate tabu ya kufata huduma mbali na maeneo yao.