JKCI YAANZISHA HATUA MPYA HUDUMA ZA TIBA KUPITIA KITUO CHA TIBA YA MICHEZO
Posted on: July 10th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF – Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, amesema Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuwa tegemeo la huduma za kibingwa za moyo nchini kwa kutoa matibabu ya kisasa na kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Bw. Rumatila amesema hayo leo Julai 10, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Tiba ya Michezo kwa ajili ya maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), iliyofanyika katika Hospitali ya Dar Group, jijini Dar es Salaam.
Amesema ujenzi wa Kituo cha Tiba ya Michezo unaashiria hatua mpya ya kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu kwa wanamichezo, pamoja na kukuza elimu, utafiti na ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya. Aidha, kituo hicho kitaiwezesha Tanzania kuwa na huduma bora zaidi wakati wa AFCON 2027 na kuimarisha jitihada za kukuza tiba utalii.
"Leo hatuweki tu jiwe la msingi, bali tunafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya huduma za moyo nchini. Tunajenga uwezo mpya wa uchunguzi na matibabu kwa wanamichezo, tunaimarisha huduma za kinga na elimu ya afya, na tunaweka msingi wa Tanzania kuwa kitovu cha huduma bora za tiba kuelekea AFCON 2027," amesema Bw. Rumatila.
Amesema kuwa, Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kwa kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu nchini. Amesema huduma za dharura zimeongezeka kutoka vituo saba hadi 125, wodi za watoto wachanga kutoka 80 hadi 438, huku vituo vya upasuaji wa dharura vikiongezeka kutoka 445 hadi 630.
Aidha, amesema uwekezaji huo umechangia kuboresha viashiria vya afya nchini, ikiwemo kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2022.
Bw. Rumatila amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, Serikali imeongeza vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 10,153 hadi 13,683. Vilevile, hospitali 10 mpya za rufaa za mikoa zimejengwa, huku hospitali kongwe 50 zikifanyiwa ukarabati, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha