IMARISHENI MIFUMO KUSOMANA ILI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: September 27th, 2024Na. WAF, Kilimanjaro
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, amewataka watumishi wa afya kuimarisha mifumo kusomana ili kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Bw. Rumatila ameyasema hayo leo Septemba 27, 2024 alipokuwa akifanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi, Mkoani Kilimanjaro akilenga kuangalia hali ya utoaji huduma na kusisitiza uboreshaji wa mifumo ya afya pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akisisitiza kuwa wananchi ndio waajiri wao wakuu.
Katika ziara hiyo, Bw. Rumatila ameainisha hatua kadhaa zinazochukuliwa na wizara kwa lengo la kuboresha huduma, ikiwemo kuanzishwa kwa kitengo cha uchujaji damu (dialysis) ili kuwahudumia wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya figo.
Aidha, ameongeza kuwa miradi ya maendeleo inayohusisha ujenzi wa majengo ya huduma inatakiwa kuendelea kwa kasi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki katika mazingira bora zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa amewaasa watumishi wa afya kufanya kazi kwa kushirikiana kama timu, akibainisha kuwa ushirikiano ndio msingi wa kufanikisha utoaji wa huduma bora.
Amesisitiza kuwa bila ushirikiano mzuri kati ya watumishi, huduma zitakosa ufanisi unaohitajika kwa wananchi.
Bw. Rumatila na Katibu Tawala wamesisitiza kuwa juhudi za pamoja zitawezesha hospitali za rufaa kutoa huduma bora zaidi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati na viwango vya ubora vinavyotarajiwa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha hospitali za rufaa zinatoa huduma bora kwa wananchi na kukidhi mahitaji ya afya kwa ufanisi mkubwa.