Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HONGERA WIZARA YA AFYA KWA KUONGEZA WATAALAMU WA UPASUAJI KWA MAJERUHI WA MAAFA YA KATESH

Posted on: December 4th, 2023

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameipongeza Wizara ya Afya kwa jitihada za kuongeza wataalamu wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa ajili ya kuhudumia majeruhi wa maafa ya mafuriko yaliyotokea Katesh Wilayani Hanang.

Mhe. Majaliwa amebainisha hayo leo wakati amewasili wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kukutana viongozi wa mkoa huo na wa Serikali na kupokea taarifa ya hali halisi ya tukio la maafa lililotokea jana na kusababisha vifo na majeruhi.

Waziri Mkuu ametoa pole kwa viongozi na wananchi wa Hanang kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumatatu, Desemba 4, 2023) kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, vyombo vua ulinzi na usalama na Watendaji wa taasisi za Serikali.

Mhe. Majali amesema tukio la jana linafanana na tukio jingine lililowahi kutokea mwaka 1990 katika eneo la Ndanda ambako mlima uliporomoka na kusomba nyumba na barabara, hali ambayo ilisababisha vifo na majeruhi.

Amezishukuru Kamati za Maafa za Wilaya na Mkoa ambazo zilianza kuchukua hatua za uokoaji tangu jana, lakini pia mawaziri na watendaji wao ambao walikuja kutoa msaada kwa kuungana na viongozi wa mkoa wa Manyara.

Amesema matibabu yanaendelea kutolewa kwa majeruhi ambapo timu ya madaktari bingwa kutoka Dodoma, Singida na Arusha imeungana na kuanza kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa watatu waliovunjika mifupa.

Amesema majeneza yameagizwa kutoka Babati na Singida ili ndugu waliotambuliwa waweze kuhifadhiwa kwenye nyumba zao za milele.

Hivi sasa, Mhe. Majaliwa na baadhi ya mawaziri wamekwenda kukagua eneo la Mlima Hanang kwa kutumia helikopta. Eneo hilo ndiko maporomoko ya udongo yalianzia. Baadaye atashiriki kuaga miili ya marehemu na ndipo taarifa rasmi itatolewa.