Wizara Ya Afya

HARAMBEE UPANDIKIZAJI FIGO, ULOTO KUFANYIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Posted on: March 31st, 2026


Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma 


Hospitali ya Benjamin Mkapa imepanga kufanya harambee kwa ajili ya kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Selimundu (sickle cell) na kusaidia matibabu ya upandikizaji Figo kwa wananchi wenye uhitaji,katika  kuelekea maadhimisho ya kutimiza miaka 10 ya hospitali hiyo. 


Kauli hiyo imetolewa tarehe 31 Machi,2026 na  Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Prof. Abel Makubi,wakati akiongea na wanahabari na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka kumi ya Hospitali hiyo,ambapo ameeleza  kilele chake kimepangwa kufanyike tarehe 8 Mei, 2026. 

 

"Jambo hili tunalifanya Sisi Benjamin Mkapa  kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), matibabu ya upandikizaji Figo na Uloto yanahitaji gharama kubwa sana, hivyo ni vigumu  kwa Mtanzania wa kipato cha chini kumudu gharama hizo," amesema Prof. Makubi


Amesema, Mgeni Rasmi katika harambee hiyo anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ameeleza kuwa Kwa upande wa Zanzibar harambee  inatarajiwa kufanyika   tarehe 11 Aprili, 2026 ambapo Jumla ya Shilingi Billion 7 zinatarajiwa kukusanywa. 


Aidha, Prof. Makubi amesema hadi sasa, idadi ya watoto 28 wamepatiwa huduma hiyo,Watanzania wakiwa 27 na mtoto mmoja (1) kutoka nchi ya  Congo DRC kwa gharama ya  shilingi Bilioni 1.9, ambapo jumla ya shilingi Bilioni 1.3 zimeokolewa  kama  matibabu haya yangefanyika nje ya nchi. 


"Hospitali kwa sasa ina hudumia wananchi kama Mil. 10 hivi,Na Kwa  sasa  Hospitali ina  Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi  zaidi ya  100 na  inatoa huduma 20 za Ubingwa na 18 za Ubingwa Bobezi," amesema Prof. Makubi 


 Prof. Makubi ametoa wito kwa Mashirika, Taasisi, Makampuni,wadau mbalimbali pamoja na   Wananchi  kushiriki katika kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto na upandikizaji Figo kwa wananchi wenye uhitaji kwa kuchangia fedha kupitia Control Namba 995220798235 Kwa Jina: 'BMH Organ Transplant au Account" Namba 102501000407 (BOT) Jina: BMH Organ Transplant. 


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt. David Mwenesano aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Mfuko huo amesema, mfuko huo unatambua kuwa, huduma za matibabu ya upandikizaji Figo na Uloto ni ya gharama kubwa hasa ukizingatia kuwa matibabu haya hayapo kwenye vifurushi vya BIMA ya Afya (NHIF).


"Bado vifurushi vya NHIF, havijaanza kugharamia matibabu ya kupandikiza Uloto na Figo badala yake , Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi  kwa ajili ya kusaidia Watanzania wasio na uwezo na wenye kuhitaji huduma hii muhimu," amesema Dkt. Mwenesano