Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA EPIDEMIOLOJIA NI NGUZO MUHIMU YA KUDHIBITI MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NCHINI

Posted on: July 24th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya katika epidemiolojia ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na kuimarisha mifumo ya afya nchini, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema hayo Julai 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya wahitimu 20 wa kundi la kwanza la mafunzo ya SPARK–NCD Short Course in Epidemiology, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe.

Amesema wahitimu hao wamepata uwezo wa kutumia ushahidi wa kisayansi na takwimu kuboresha huduma za afya, jambo litakalosaidia nchi kugundua na kudhibiti magonjwa mapema.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takribani asilimia 39 ya vifo vyote nchini Tanzania, huku magonjwa ya moyo, saratani, kisukari na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji yakiendelea kuwa changamoto kubwa.

Bw. Tayari amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeongeza uwekezaji katika miundombinu ya afya, vifaa tiba, huduma za kibingwa, uzalishaji wa bidhaa za afya na maendeleo ya rasilimali watu.

Aidha, amesema Wizara ya Afya chini ya Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC), huduma za afya msingi, mifumo ya kidijitali na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania, Africa CDC, MUHAS, AFENET, WHO na wadau wengine katika kujenga uwezo wa kugundua na kudhibiti magonjwa yanayoweza kuvuka mipaka ya nchi.

Akihitimisha, Bw. Tayari amewataka wahitimu kutumia takwimu na ushahidi sahihi katika kufanya maamuzi ya afya, akieleza kuwa matumizi ya takwimu zisizo sahihi yanaweza kusababisha maamuzi yanayoathiri maisha ya wananchi.