TIMU YA UTAYARI WA DHARURA KUWA CHACHU KWENYE DHARULA NA MAJANGA- DKT. KAGYA
Posted on: September 7th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF- Mwanza
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Kheri Kagya amesema mafunzo hayo yatawezesha kuundwa kwa timu itakayosaidia kutathmini utayari wa Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla katika kukabiliana na dharura, kubaini maeneo yenye changamoto na kupendekeza hatua za kuyaimarisha ili huduma za afya zitolewe kwa haraka wakati wa majanga.
Dkt. Kagya ameyasema hayo leo Septemba 7, 2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayo tarajiwa kuendeshwa kwa sıku tano jijini Mwanza.
Amesema mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kukabiliana na dharura kwa ufanisi kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kimataifa.
"Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) za kuwajengea uwezo wataalamu wa afya juu ya kanuni na viwango vya uendeshaji wa Timu za Dharura za Matibabu (Emergency Medical Teams EMT), mwitikio wa dharura za afya na ushirikiano wa kitaalamu wakati wa kutumwa ndani ya maeneo yaliyoathiriwa na majanga", amesema Dkt. Kagya.
Dkt. Kagya ameongeza kuwa uwepo wa wataalamu wenye ujuzi wa kuitikia dharura kwa haraka utasaidia kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga na kuhakikisha mwendelezo wa huduma za afya kwa wananchi.
“Mnaandaliwa kuwa tayari kutoa msaada ndani na nje ya nchi katika masuala ya dharula na majanga.” Amesema Dkt. Kagya
Ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya na WHO kwa ushirikiano na kuwezesha mafunzo hayo, akisema yataimarisha mifumo ya mwitikio wa dharura, kuongeza utayari wa wataalamu na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.