Wizara Ya Afya

SERIKALI YAONGEZA WATUMISHI, UWEKEZAJI MIUNDOMBINU SEKTA YA AFYA

Posted on: September 9th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF – Arusha

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi na kuongeza idadi ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Dkt. Mwigulu amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi jijini Arusha, na kusema kuwa uwekezaji huo umelenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema jitihada hizo zimeendelea kuongeza mvuto wa wananchi kutumia vituo rasmi vya kutolea huduma za afya, hali inayochangia kuimarika kwa upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Aisha amesema kuwa serikali inatambua umuhimu wa kukidhi mahitaji ya wataalamu wa afya, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi na kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa uwekezaji katika sekta ya afya unakwenda sambamba na utekelezaji wa miradi mingine mikubwa ya kimkakati ya Serikali, ambayo ikikamilika itawezesha Serikali kuongeza kasi ya kufanya maboresho zaidi katika huduma za kijamii, ikiwemo afya.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuyatekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo katika maboresho ya huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kujali maeneo wanayoishi au uwezo wao wa kiuchumi.

Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kujikita kwenye majadiliano na kuweka malengo yanayotekelezeka, ili mapendekezo yatakayokubaliwa yaweze kuleta matokeo yanayoonekana katika mifumo ya afya.

Amesema mafanikio ya afya ya msingi yanahitaji ushirikiano wa Serikali, wadau wa maendeleo, wataalamu wa afya na wananchi ili kuhakikisha huduma bora, endelevu na zenye usawa zinapatikana kwa wote.