Wizara Ya Afya

AFRIKA YAHIMIZWA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA KIAFYA

Posted on: September 9th, 2026

Na. Aisha Swahibu, WAF - Arusha

Afrika imehimizwa kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya msingi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma sahihi, mahali sahihi na kwa wakati sahihi, kabla hali zao za kiafya hazijafikia hatua ya kuhatarisha maisha.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Ukanda wa Afrika Prof. Mohamed Yakub Janabi wakati wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (PHC), 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha, leo Septemba 9, 2026

Amesema uzoefu wake wa kuwahudumia wagonjwa wenye hali mbaya umeendelea kumfanya kujiuliza iwapo wagonjwa hao wangepata huduma mapema katika vituo vya afya vilivyo karibu na maeneo wanayoishi, huenda baadhi yao wasingefikia hatua ya kuwa na hali mbaya.

Dkt. Janabi ameeleza kuwa huduma za afya ya msingi si suala la kuwa na zahanati pekee, bali ni mfumo unaohakikisha huduma sahihi zinapatikana kwa wakati na karibu na wananchi huku akisisitiza kuwa mifumo imara ya afya ya msingi ina nafasi kubwa katika kugundua magonjwa mapema, kuzuia milipuko, kuendelea kutoa huduma muhimu wakati wa majanga na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na changamoto za kiafya.

Aidha, Dkt. Janabi amesema changamoto za kupungua kwa ufadhili wa afya na athari za janga la COVID-19 zimeonesha umuhimu wa kuwa na mifumo ya afya yenye uwezo wa kustahimili misukosuko.

Ameongeza kuwa nchi zenye mifumo imara na inayobadilika ya huduma za afya ya msingi ziliweza kuendelea kutoa huduma muhimu hata katika vipindi vya majanga.