Wizara Ya Afya

SEKTA BINAFSI KUENDELEA KUSHIRIKISHWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: September 9th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo kujifunza na kutumia uzoefu wa sekta hiyo katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Dkt. Magembe amesema hayo leo Septemba 09, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha, wakati akizungumza katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (PHC), 2026.

Amesema, ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa sekta binafsi imeendelea kuwa na uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo namna ya kuwahudumia wananchi, matumizi ya mifumo ya kidijitali na uboreshaji wa uzoefu wa mteja.

“Serikali imejifunza mengi kutoka sekta binafsi, tunachokifanya sasa ni kuhakikisha mifumo iliyopo katika sekta binafsi na ile ya Serikali inaweza kuwasiliana kupitia mfumo wa 'interoperability',” amesema Dkt. Magembe

Amesema, Serikali pia inaendelea kupunguza idadi ya mifumo mbalimbali ya kidijitali katika sekta ya afya ili kuhakikisha mifumo iliyopo inaweza kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi, hatua itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma.

Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali inaendelea kuandaa Kituo cha Taifa cha Takwimu za Afya (Health Data Centre), kitakachosaidia kukusanya na kuunganisha taarifa za afya kutoka vyanzo mbalimbali, hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa kutoka chanzo kimoja kwa matumizi ya tafiti, majaribio ya kitabibu na shughuli nyingine za kitaalamu.

Katika upatikanaji wa taarifa hizo, Dkt. Magembea amesema utazingatia majukumu na viwango vya uhitaji wa watumiaji, huku hatua hiyo ikiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha matumizi ya teknolojia, takwimu na ushirikiano na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.