UPASUAJI WA USO, KINYWA NA MENO WAFANYIKA KWA MAFANIKIO KAMBI YA MADAKTARI BINGWA MTWARA
Posted on: July 24th, 2026Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wanaoshiriki katika kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ECSA-HC, wamefanikiwa kufanya upasuaji wa uso, kinywa na meno kwa mgonjwa aliyejeruhiwa katika Hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini-Mtwara, ikiwa ni sehemu ya huduma za kibingwa zinazoendelea kutolewa katika kambi hiyo iliyofunguliwa rasmi Julai 20, 2026.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa upasuaji huo, Dkt. Mohamed Mkawa, Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji wa Uso, Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, amesema upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio kwa ushirikiano na madaktari wengine, huku mgonjwa akiendelea kuwa katika hali salama.
“Upasuaji umefanyika vizuri na mgonjwa yuko salama. Tumefanya kazi kwa ushirikiano na madaktari wengine, na ushirikiano huu ni muhimu katika kuhakikisha mgonjwa anapata huduma bora na salama,” amesema Dkt. Mkawa.
Aidha Dkt. Mkawa ameongeza kuwa kambi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi kwa kuwa inasogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, hivyo kuwasaidia kupata matibabu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu, jambo linalosaidia kupunguza gharama za usafiri, malazi na matibabu.
Hata hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kufanya jambo muhimu kwa kuandaa kambi hiyo kwa kushirikiana na ECSA-HC, kwani ushirikiano huo umewezesha upatikanaji wa Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji matibabu ya kibingwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mkawa, hadi Julai 24, 2026, timu ya wataalamu wa Upasuaji wa Uso, Kinywa na Meno ilikuwa imefanikiwa kuwaona takribani wagonjwa 30 wa kinywa huku wengine zaidi ya 100 wakifanyiwa vipimo vya awali hata hivyo amewataka wananchi wenye changamoto zinazohusiana na huduma hizo kutumia fursa hiyo kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
“Ninawahamasisha wananchi waje kupata huduma hizi kwa sababu ni muhimu na zinapatikana hapa karibu. Mtu mwenye changamoto ya uso, kinywa au meno asisite kufika hospitalini ili aweze kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu stahiki,”