Wizara Ya Afya

TANZANIA, MAREKANI KUIUNGANISHA AFRIKA KWENYE SEKTA YA AFYA

Posted on: September 4th, 2026

Na John Mapepele, WAF-Washington, D.C

Serikali ya Tanzania imekubaliana na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani (U.S. Chamber of Commerce) mjini Washington, D.C na Serikali ya Marekani kufanya utekelezaji wa kimkakati wa mkataba wa sekta ya afya ulioingiwa hivi karibuni ili kuzinufaisha pande zote mbili,huku wakiifanya Tanzania kuwa muhimili wa uzalishaji na usambazaji dawa na vifaa tiba katika bara la Afrika.

Akizungumza leo Septemba 4,2026 kwenye Mkutano wa Wadau wa Ushirikiano wa Afya kati ya Marekani na Tanzania uliofanyika kati ya Serikali ya Tanzania na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani (U.S. Chamber of Commerce) mjini Washington, D.C., na baadaye kufanya kikao viongozi waandamizi Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Waziri wa Afya wa Tanzania, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, alifafanua kuwa tayari Tanzania imejipanga vema kuhakikisha mkataba unatekelezwa kikamilifu.

Akielezea zaidi kuhusu mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya dawa amesema Tanzania inafanya kazi ya kuoanisha utaratibu wa kutoza kodi na ushuru kwa malighafi na vifungashio vya dawa na mifumo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa lengo la kufanya uzalishaji wa ndani uwe na ushindani zaidi kuliko kuagiza bidhaa zilizokamilika kutoka nje.

Pia amesema,Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji na kiongozi wa Huduma za Ununuzi wa Pamoja za SADC (SADC Pooled Procurement Services), mpango unaolenga kuunganisha mahitaji ya dawa na bidhaa za afya katika nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Hili linaunda fursa yenye nguvu kwa wazalishaji.

Badala ya kuanzisha uzalishaji nchini Tanzania kwa lengo la kuhudumia soko la takribani watu milioni 60 pekee, wawekezaji wanaweza kuitumia Tanzania kama kituo cha uzalishaji na usambazaji kwa soko la kikanda linalojumuisha nchi 16 za SADC na zaidi ya watu milioni 300.

Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji makini kutoka Marekani na ipo tayari kupokea mtaji, teknolojia.