Wizara Ya Afya

SERIKALI YAKAMILISHA UKAGUZI MAENEO YA UJENZI WA VITUO VYA ISOLATION KATIKA MIPAKA 13 YA TANZANIA.

Posted on: July 24th, 2026

Na Abdu Madenge, WAF | Pemba, Zanzibar

Serikali kupitia Wizara ya Afya imekamilisha zoezi la ukaguzi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Isolation na Temporary Holding Facilities katika vituo vya kutolea huduma za afya mipakani, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa nchi wa kuzuia, kugundua na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza yanayoweza kuvuka mipaka.

Zoezi hilo lilifanyika kuanzia Julai 14 hadi 23, 2026, likihusisha timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya waliotembelea vituo mbalimbali vya afya mipakani ili kukagua na kuthibitisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza Julai 24, 2026 akiwa Pemba, Zanzibar, Msanifu Majengo wa Wizara ya Afya, Arch. James Mbellah, alisema ukaguzi huo ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa miundombinu hiyo kupitia Idara ya Kinga, Sehemu ya Afya ya Mazingira na Usafi, chini ya Sehemu Ndogo ya Huduma za Afya Mipakani, ambayo inasimamia utoaji wa huduma za uchunguzi wa afya kwa wasafiri katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu.

Alisema huduma hizo ni muhimu katika kudhibiti kuingia au kutoka nchini kwa magonjwa ya kuambukiza pamoja na kukabiliana na matukio mengine ya dharura ya afya ya umma, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa Kanuni za Kimataifa za Afya (International Health Regulations – IHR).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Amour Seleman, wakati wa kuanza kwa zoezi hilo, utambulisho wa wataalamu na ukaguzi wa maeneo hayo ulikuwa sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na Pandemic Fund, unaolenga kuongeza uwezo wa Tanzania wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa afya mipakani.

Aidha, alieleza kuwa miongoni mwa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya mipakani ni uchunguzi wa awali wa afya kwa wasafiri (health screening), unaosaidia kubaini mapema vihatarishi vya kiafya na kuzuia kusambaa kwa magonjwa yanayoweza kuathiri afya ya jamii.