Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA INA DHAMANA KUBWA KWA TAIFA KUWA NA AFYA BORA

Posted on: June 25th, 2024

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewakumbusha wajumbe wa menejiment ya Wizara dhamana ya jukumu la kuhakikisha Taifa la Tanzania linakuwa na Afya bora siku zote.

Dkt. Jingu ameyasema hayo leo Juni 25, 2024, jijini Dodoma wakati akifungua semina elekezi kwa wajumbe wa menejimenti ya Wizara ya Afya yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhakikisha wizara inafikia malengo yake unapoingia mwaka mpya wa fedha 2024/25.

Amesema Menejimenti na Watumishi wa sekta ya Afya wanatakiwa kujua dhamana hiyo kubwa waliopewa na serikali hivyo wanatakiwa kujipanga vizuri ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Wakati tunapomaliza mwaka wa fedha na kuingia mwaka mpya tunapaswa kujikumbusha kuwa afya ndio msingi wa taifa lolote na mtu binafsi, Wizara imekabidhiwa kazi ya kusimamia afya za watu hivyo sisi ni timu, tunatakiwa kwenda pamoja ili kutekeleza jukumu la Taifa letu kuwa na afya bora muda wote”. Amesema Dkt. Jingu.

Ameongeza kuwa kila mtumishi wa sekta ya Afya anatakiwa kuwa msimamizi mzuri wa usalama wa afya nchini unaopelekea kulinda hadhi ya Serikali na Wizara.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amemshukuru Katibu Mkuu Dkt. John Jingu kwa kuwajengea utamaduni ambao utakuwa endelevu ndani ya Wizara ambao utakuza mitanzamo ya Wizara.

“Katibu Mkuu Dkt. Jingu amekuwa akichukua hatua za kutuelimisha zaidi kuliko kutoa maelekezo hii inatujengea utamaduni mzuri ambao tunaamini utakuwa endelevu hadi kwa viongozi wa menejimenti wajao”


Mwisho.