Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATUMIENI MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUBORESHA UTENDAJI WENU

Posted on: October 10th, 2024

Na WAF, TABORA

Mratibu wa zoezi la Madaktari Bingwa na Bobezi katika mkoa wa Tabora Dkt. Eveline Maziku amewataka watumishi wa afya kwenye mkoa huo kuzingatia maelekezo
yanayotolewa na Mabingwa hao.

Dkt. Maziku ametoa rai hiyo Oktoba 10,2024 wakati wa zoezi la ufuatiliaji lilioanza Jumatatu ya wiki hii na kutarajiwa kukamilika Oktoba 12, 2024 katika wilaya zote nane za mkoa wa Tabora.

Akizungumza kwa nyakati tofauti Dkt. Maziku amesema zoezi hilo la utoaji wa huduma linalokwenda sambamba na kuwajengea uwezo watumishi ni muhimu kwa maslahi mapana ya afya za watanzania hasa katika ngazi ya msingi.

"Watumieni ipasavyo hawa madaktari Bingwa, maana shughuli yao hapa mbali na kutoa huduma pia wanawajengea uwezo, msiwaache waondoke na maarifa
walioyokuja nayo bila kuelewa," amesisitiza Dkt. Maziku.

Kwa upande wao watumishi hao wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye Halmashauri za Igunga, Nzega Mji na Nzega Wilaya pamoja na Uyui wameeleza kuwa wamezingatia maelekezo hayo.

"Tulichokifanya hapa Igunga Halmashauri sio tu kuwajengea watumishi wa hapa Hospitali ya wilaya, lakini pia tumechukua na wale wa vituo vya jirani," ameeleza Elizabeth Mpangala Katibu wa Hospitali ya Wilaya Igunga.

Naye Tumaini Fumbuka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Uyui, amesema mbali na kuwajengea uwezo wakati wa kuchukua historia za wagonjwa lakini wanahakikisha wanapita nao wodini kujua maendeleo ya mgonjwa, hali inayowajenga zaidi kujua mchakato mzima wa kumhudumia mgonjwa.

Kambi ya Madaktari Bingwa katika mkoa wa Tabora mbali ya kutoa huduma imefanikisha pia kuanzisha huduma za upasuaji kwa Hospitali za wilaya za Sikonge na Uyui ambazo zilikuwa na vifaa lakini zilikuwa hazijaanza kutoa huduma hiyo.