Ministry of Health

WATAALAM IRINGA DC WAIWEKA JAMII NA UTAYARI DHIDI YA EBOLA NA ATHARI ZA EL NIÑO

Posted on: September 24th, 2026

Na Atley Kuni, WAF- Iringa DC

Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeendelea kuimarishwa juu ya utayari na uelewa wa wataalamu wake kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola pamoja na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha.

Zoezi hilo ni sehemu ya ziara ya uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii inayofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wadau wa maendeleo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na TIP.

Katika ziara hiyo, timu imefika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kukutana na wataalamu wa Halmashauri (CHMT), ambapo imeendesha zoezi la kujaza na kupitia maswali ya dodoso yanayolenga kupima na kuimarisha uelewa kuhusu maafa, milipuko ya magonjwa na athari zake.

Zoezi hilo pia linalenga kuimarisha hatua sahihi za kujikinga na magonjwa, kuongeza utayari wa Halmashauri hiyo juu ya kukabiliana na dharura na maafa, pamoja na kuimarisha uratibu wa shughuli za elimu ya afya katika ngazi ya Halmashauri na jamii.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa zoezi hilo, Septemba 24, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw. Robert Masunya, ametoa wito kwa wataalamu wote wanaohusika kuhakikisha wanajibu dodoso hilo kwa umakini, uadilifu na usahihi, kwa kuwa taarifa zitakazopatikana zitasaidia kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa na hatimaye kuongeza ufanisi wa hatua za kinga na mwitikio.

Masunya amesisitiza kuwa ushiriki wa wataalamu katika zoezi hilo si suala la kujaza dodoso pekee, bali ni sehemu ya maandalizi muhimu ya Halmashauri ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na wanapata elimu sahihi kwa wakati.

“Natoa wito kwa wataalamu wote kujibu dodoso hili kwa umakini na kutoa taarifa sahihi ili ziwe na manufaa katika kupanga na kuchukua hatua zinazolenga kuwalinda na kuwahudumia wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa ufanisi zaidi” amesema Masunya.