Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATAALAM BINGWA NA BOBEZI WA AFYA 28 WAPOKELEWA RUKWA KWA KISH8NDO

Posted on: September 30th, 2025

NA WAF – RUKWA

Timu ya Wataalam na Madaktari 28 Bingwa na Bobezi wamewasili mkoani Rukwa na kupokelewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Ibrahim Isack kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa Halmashauri zote za mkoa huo kwa muda wa siku sita.

Akizungumza leo, Septemba 29, 2025, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere, Mgamga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Isack amewakaribisha madaktari hao na kusisitiza umuhimu wa kazi wanayoifanya ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Mnapokuja katika mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kuboresha uwezo wa watumishi, tunajenga imani kwa wananchi kuwa Serikali yao inawathamini. Hivyo niwaombe kuifanya kazi hii kwa uaminifu na bidii,” amesema Dkt. Isack.

Aidha, Dkt. Isack amesema mkoa umejipanga kikamilifu kwa kufanya uhamashishaji katika Halmashauri zote na wananchi wameanza kujiandikisha kwenye hospitali zilizoteuliwa.

Ameongeza kuwa muitikio wa wananchi ni mkubwa na matarajio ni kwamba wengi watanufaika na huduma hizo ambazo zitapunguza gharama za kusafiri kwenda hospitali za Kanda na Taifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Bi. Jesca Masanja, Afisa Programu kutoka Idara ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto, amesema malengo makubwa ya ujio wa madaktari hao ni kutoa huduma za kibingwa na kujenga uwezo kwa wataalam wa afya katika maeneo yao ya kazi ili kupunguza rufaa zisizo za lazima.