Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANAWAKE TUMIENI FURSA ZA UWEZESHAJI KIUCHUMI, ACHANENI NA KAUSHA DAMU- MAKINDA

Posted on: March 3rd, 2025

Na. WAF, Dodoma


Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anna Makinda ametoa wito kwa wanawake nchini kuhakikisha wanatumia kikamilifu fursa za uwezeshaji kiuchumi na mikopo yenye riba na masharti nafuu ili  kufikia lengo la kujiinua kiuchumi.


Mhe. Makinda ameyasema hayo Machi 03, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kongamano la Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani. 


“Niwasisitize wanawake wote kuhakikisha mikopo inayotolewa kwenu iwe yenye tija na na siyo ile ya kausha damu, kila mkoa una fursa hawa wakuu wa mikoa wanafahamu mengi hivyo acha kukata tamaa na kusikitika bali nendeni kwenye mabenki msiogope kwa sababu huko  pia mtafundishwa kulingana na biashara mnayotoka kufanya,” amesisitiza Mhe. Makinda. 

 

Amesema Serikali inatengeneza program ya kitaifa ya kizazi chenye usawa ya mwaka 2021/2026 ambayo imejikita kutoa msukumo wa masuala ya uwezeshaji kwa kuhakikisha inakuza haki na fursa za kiuchumi hii ni kutokana na umuhimu kwamba mwanamke akiimarika kiuchumi ni nyenzo muhimu kwake katika kumpatia uwezo wa kugombea nafasi za uongozi.


Aidha, Mhe. Makinda ametoa rai kwa wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali kuwashika mkono wanawake wengine ili kwa pamoja waweze kuinuka kwa ustawi na maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla.


“Waliopata nafasi na kufanikiwa kama sisi inabidi tushirikiane nanyi ili kuwaeleza ni changamoto na njia gani tumepitia na kufika katika nyanja za uongozi na hata kibiashara ili muweze kupata moyo wa kwenda mbele zaidi,” amesema Mhe. Makinda.


Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita (6) imeendelea kuona umuhimu wa wanawake katika jamii na ndio maana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka msaada wa kisheria, elimu na huduma za afya kwa jamii  wakiwemo wanawake na watoto.


Awali,  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizu gum za katika kongamano hilo amewataka wanawake wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi za udiwani na ubunge kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.


“Takwimu za uongozi kwa mkoa wa Dodoma zinaonyesha asilimia 71 ya wakuu wa wilaya ni wanawake ambapo katika wilaya saba za mkoa wetu wakuu wa wa wilaya wanaume ni wawili na wanawake ni watano na wanafanya vizuri, na kwa wabunge asilimia 11 ni wanawake, kwa hili linaonyesha nafasi za kuteuliwa ni wengi kuliko nafasi za kugombea hivyo nitoe rai kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema Mhe. Senyamule.