Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANANCHI WAOMBA ONGEZEKO LA MUDA KWA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA BAADA YA MUITIKIO MKUBWA

Posted on: May 10th, 2024



Na WAF, Iringa


Muitikio wa wananchi kufuata huduma za madaktari bingwa wa Rais Samia umekuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa, huku idadi kubwa ya wananchi wakijitokeza kutafuta matibabu hali iliyopelekea wananchi hao kuomba madaktari bingwa waongezewe muda wa kutoa huduma.


Hayo yamejiri Mkoani Iringa katika kambi za madaktari bingwa wa Rais Samia katika Hospitali 5 za Halmashauri katika mkoa huo ambapo madaktari hao wanatoa Huduma za Afya kwa watoto na watoto wachanga, Huduma za Afya ya Uzazi, Wajawazito na Magonjwa ya wanawake, Huduma ya Magonjwa ya ndani (Shinikizo la damu,kisukari, n.k), Huduma za Upasuaji, Huduma za Ganzi na usingizi


Awali, daktari bingwa wa afya ya uzazi na magonjwa ya kina mama Dkt. Titus Mmasi ameelezea muitikio wa wananchi kuwa ni wa kushangaza na kwamba idadi ya watu wanaohitaji matibabu ni kubwa zaidi ya walivyotarajia. 


“wanaohitaji huduma ni wengi kuliko tulivyotarajia na hii inaleta changamoto kubwa kwa kwani inatulazimu kutoa huduma mpaka saa 5 usiku lakini bado idadi ya watu ni kubwa”.Amesema Dkt. Mmasi


Aidha Wananchi wameonyesha hamu kubwa ya kupata matibabu bora kutoka kwa madaktari bingwa hao, na hivyo kuongeza shinikizo la kuongezwa kwa muda wa kutoa huduma ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kupata matibabu.


Hata hivyo wananchi hao wamesema kuwa Madaktari bingwa wa Rais Samia wamekua ni Faraja kubwa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali kutokana na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ambazo zinachagiza kuokoa Maisha ya wananchi katika mkoa wa Iringa na kupunguza adha ya gharama za matibabu.


Sambamba na hilo wameiomba serikali kutoa muda mwingi zaidi kwa madaktari hao kuweza kuhudumia jamii ama kuwaleta wengi zaidi ili kuweza kuisadia jamii.