Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANANCHI TUMIENI FURSA YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: September 23rd, 2024

Na WAF - Manyara

Wananchi wa Mkoa wa Mnyara wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa kambi ya siku sita ya matibabu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia kwa kufika katika hospitali zote za halmashauri ya zao ili kupatiwa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa na kuangalia afya zao kwa wasio na changamoto za kiafya.

Wito huo umetolewa Septemba 23, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Babati Mjini Mhe. Emmanuela Kaganda kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga wakati akiwapokea na kufungua Kambi ya Matibabu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika Hospitali ya Wilaya ya Babati Mjini, iliyowekwa katika Mkoa huo kuanzia kwa siku sita kuanzia tarehe 23 hadi 28 Septemba, 2024.

Mhe. Emmanuela amesema ni vyema kwa wananchi wa Mkoa huo kutenga muda wao na kwenda katika hospitali walipo madaktari bingwa hao na kupima afya zao kwani kujua afya yako mapema kutasaidai kupatiwa matibabu mapema na kuebukana na athari zinazoweza kuepukika kutokana na magonjwa.

Ameongeza kuwa serikali inayoongwaza na Rais Samia Suluhu Hassani inadhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za kibingwa karibu na eneo analoishi .

“Ni maono makubwa na mazuri ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi baada ya kushusha fedha nyingi na kujenga hospitali kubwa na nzuri, vituo vya kutolea huduma za Afya na zahanati katika kila mkoa na kusambaza vifaa tiba vya kisasa Pamoja na dawa ameona ni vyema kuwasongezea na kuwafikishia huduma za matibabu ya kibingwa karibu walipo watanzania na kuwatua mzigo wa gharama za matibabu wananchi hasa wa hali ya chini wasizifuate huduma hizo mbali ya maeneo yao.” Amesema Mhe. Emmanuela

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya. Bi. Gertrude Naphtali ambae ni Afisa Mbobezi Afya ya Jamii kutoka Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto amesema seti ya madaktari bingwa 45 wamesambazwa katika hospitali zote za halmashauri za Mkoa wa manyara kwa ajili ya kutoa matibabu ya kibingwa wa Watanzania na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ii kupatiwa huduma za kibingwa.