Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANANCHI BUCHOSA WAJITOKEZA KWA WINGI KUPATA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA

Posted on: November 7th, 2024

Na WAF, BUCHOSA

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Buchosa Dkt. Avelin Gabriel amesema kumekuwa na muitikio mkubwa wa wananchi kwenye kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia ambao wanafika na kupatiwa matibabu.

Dkt. Gabriel ameyasema hayo hospitalini hapo Novemba 06, 2024 ikiwa ni siku ya tatu ya kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia ambao wameendelea kutoa huduma mbalimbali za kitabibu.

"Wananchi wapatao 300 wamejitokeza ndani ya siku mbili, tunategemea idadi hiyo itaongezeka," amesema Dkt. Gabriel.

Dkt. Gabriel amefafanua kuwa imekuwa tofauti na matazamio, kwani huu ni msimu wa kilimo, hivyo walikuwa na wasiwasi na idadi ya wananchi watakaoijitokeza , jambo ambalo limekuwa tofauti kwani wengi wanaendelea kujitokeza na kupata huduma.

"Hamasa kubwa tuliyopeleka kwenye nyumba za ibada, mbao za matangazo, huduma ya kuzunguka na gari na kutangaza kwenye kata zote, ndiyo imeleta tija kwa wananchi kujitokeza, " amefafanua Dkt. Gabriel.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo Bi. Editha Buha amesema wananchi wa wilaya hiyo wana muamko wa kupata huduma za afya kwenye vituo vya afya.

" Kutokana na jiografia ya wilaya yetu kuna wakati huduma za kibingwa sio rahisi kuzifikia na ukizihitaji ni lazima uende Bugando au hospitali ya kanda Chato, hivyo ujio huu kwetu umekuwa ni jambo lenye tija kwa afya za wanabuchosa," amesema Bi Buha.

Akizungumza hospitalini hapo mmoja ya wananchi waliofika kwa huduma za kitabu Bi. Methusela Masunga, hakusita kuonesha furaha yake na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea huduma za kibingwa.

"Mara ya mwisho nilipokuja niliambiwa madaktari bingwa wameshaondoka lakini niliambiwa wangerudi tena, hivyo jumapili tulivyotangaziwa kanisani nikaona nitumie nafasi hii adhimu," amesema Bi. Masunga.