WANANCHI 319 KAHAMA WATIBIWA NDANI YA SIKU MBILI
Posted on: November 7th, 2024
Na WAF - Kahama
Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, imetoa huduma ya matibabu kwa wananchi 319 ndani ya siku mbili na kuleta faraja kwa wakazi wa manispaa hiyo.
Akizungumzia ujio huo leo Novemba 6, 2024 Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Sospeter Boyo, amesema kuwa madaktari bingwa hao wameleta faraja kubwa kwa wananchi wilayani humo, kwani wengi wanaendelea kujitokeza na kupata huduma.
"Kwakweli uwepo wa kambi hii ya madaktari bingwa imekuwa faraja sana kwetu kwa sababu kuna baadhi ya matatizo makubwa tulikuwa hatuwezi kuyatatua lakini kwa ujio huu wananchi wanatatuliwa matatizo hayo hospitalini hapa," amesema Dkt. Bayo.
Dkt. Boyo amesema pia kama hospitali wanapata fursa ya kujengewa uwezo wa kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na madaktari ili huduma hizo ziwe endelevu katika hospitali hiyo.
"Tunaimani kuwa utaalamu na ushauri wanaotupatia madaktari hawa, baada ya kuondoka watakuwa wametujengea uwezo mzuri wa kuendelea na wagonjwa ambao watakuwa wanafika kwetu," amesema Dkt. Boyo.
Aidha Dkt. Boyo amewaomba wananchi wote wa manispaa hiyo kuendelea kujitokeza kwa wingi hospitalini hapo ili kunufaika na ujio wa madaktari hao ambao watahitimisha kazi hiyo ifikapo Novemba 9, 2024.
Naye Bi. Catherine Restuta mkazi wa Kahama ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea huduma hizo za kibingwa karibu na kufanya gharama ya matibabu kuwa nafuu.