Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WALIMU WAHIMIZWA KUTAMBUA UMUHIMU WA JUKWAA LA MALEZI

Posted on: October 25th, 2023

Na WAF - Kongwa, Dodoma  


Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema amewasihi waratibu wa jukwaa la JIKUBALI kuhimiza walimu wa shule za Msingi na Sekondari kutambua umuhimu wa jukumu la malezi walilokabidhiwa ili waweze kuwa mfano wa kuigwa katika mapambano dhidi ya VVU.


Mhe. Remedius amesema hayo Oktoba 25, 2023 wakati wa uwasilishwaji wa ujumbe kutoka Jukwaa la JIKUBALI ukiongozwa Godfrey Obonyo ambaye ni afisa Elimu na mawasiliano ya kubadili tabia kutoka Mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI Wizara ya Afya ulipowasili Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma. 


Mhe. Remedius wakati akiendelea kuwasilisha ujumbe huo amesema lengo ni mwendelezo wa maandalizi ya uwasilishaji wa programu za jukwaa la JIKUBALI Wilayani hapo ili kuondoa tatizo la baadhi ya walimu kutembea na wanafunzi katika Wilaya hiyo.


“Kwenye Wilaya yangu kuna baadhi ya walimu wana kesi ya kutembea na wanafunzi na wengine kutuhumiwa kubaka wanafunzi, ni mambo yanayo sikitisha lakini yapo na lazima tuyaseme, tutawafundisha vijana na wanafunzi wataelewa lakini kama tusipowafundisha na walimu wao wanaowafundisha baadhi yao watawakengeusha”. Amesema Remidius. 


Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo Afisa Elimu na Mawasiliano ya kubadili tabia kutoka mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI Wizara ya Afya Bw. Godfrey Obonyo amesema kupitia jukwaa hilo wameazimia kuja na mafunzo maalum hasa kwa walezi na waelimishaji wa kada zote kwa kila Mkoa ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.  


Ujumbe wa Jukwaa la JIKUBALI umeambatana na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Afya, Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR- TAMISEMI ambapo kikao hicho kilihudhuliwa na wataalamu wengine kutoka Wilaya ya Kongwa akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya na Afisa Elimu Sekondari.