Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAGONJWA ZAIDI YA 3000 WAHUDUMIWA KWA SIKU TANO, KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA SAMIA

Posted on: May 10th, 2024


Na WAF - Morogoro.


Wagonjwa zaidi ya 3000 wamepatiwa Matibabu kupitia kambi ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi wa Rais Samia iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kuanzia Mei 6 hadi 10, 2024.


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima Mei 10, 2024 wakati wa hafla yakuhitimisha kambi ya Matibabu ya Madaktari bingwa na ubingwa bobezi wa Rais Samia kwa kanda ya Mashariki.


Mhe. Malima amesema idadi hiyo ya watu imechagizwa na uhitaji mkubwa wa huduma za matibabu kwa wananchi ambapo taarifa zilizopatikana kupitia kambi hiyo zitawezesha kupanga mikakati ya kupambana na magonjwa yanayowasumbua wananchi katika eneo hilo.


“ Niwapongeze kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuona idadi kubwa ya wagonjwa hii ni ishara kuwa watanzania wengi wanasumbuliwa na maradhi mbali mbali lakini walikosa fursa kama hii"  amesema Mhe. Malima


Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa Kambi ya Matibabu ya Madaktari bingwa hao ambae pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi Dkt. Amani Malima , amesema, kupitia kambi hiyo wameweza kufanyia upasuaji wagonjwa 109 huku kitengo cha Magonjwa ya ndani  kikiongoza  kuona wangojwa wengi zaidi.


“ Tunashukuru wananchi wameweza kujitokeza kwa wingi, pia tumeweza kutoa Rufaa kwa wagonjwa 34 kwenda kwenye Hospitali za Kanda na Taifa.”Ameeleza Dkt. Amani.


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi kwa mkakati huu wakuwasogezea wananchi huduma kupitia Madaktari Bingwa.


Mwisho.