Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UNDENI MIONGOZO INAYOTEKELEZEKA ILI IWAJENGE UWEZO WATUMISHI NA WANAFUNZI VYUO VYA AFYA

Posted on: January 30th, 2024


Na: WAF - Morogoro

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Wizara ya Afya, Bi. Ziada J. Sellah, amesisitiza umuhimu wa kuundwa kwa miongozo inayotekelezeka kwa ufanisi ili kujenga uwezo wa watumishi na wanafunzi wa vyuo vya afya kwa lengo la kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kupitia kitita cha mafunzo kwa wakufunzi kwa vitendo Mkoani Morogoro, Bi. Ziada ameeleza kuwa baadhi ya wahitimu hawana uwezo wa kutosha wanapofika kazini. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kupeleka wakufunzi kwa vitendo kuanzia ngazi ya vyuo hadi vituo vya huduma za afya ili kujenga uwezo wao.

Aidha, amesisitiza kuwa mafunzo yanapaswa kugusa kada zote katika sekta ya afya, kutoka kwa watumishi wa juu mpaka wale wa chini, kama vile walinzi. Hii ni kwa sababu kila mtu katika mfumo wa afya ana jukumu muhimu katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

“Mhe. Waziri na Katibu mkuu walisema hatuwezi kuishia kwa wauguzi tu kuwajengea uwezo ni vyema tushuke hadi chini kwa mlinzi kwa sababu yeye ndo mtu wa kwanza kumpokea mgonjwa getini, hivyo hii miongozo ilenge kuwagusa kada zote” amesema Bi. Ziada.

Bi. Ziada amehimiza pia kufanyika kwa mafunzo ya utangulizi kwa wafanyakazi wapya wanapoanza kazi ili kuhakikisha wanakumbushwa miongozo ya kazi kwani itasaidia kuhakikisha kuwa watumishi wanaoingia kazini wanafahamu na kuzingatia miongozo inayohitajika katika kutoa huduma za afya.

Bi. Ziada amesisitiza umuhimu wa kuweka mkazo katika mafunzo ya mara kwa mara ili kuhakikisha watumishi wa afya wanabaki katika kiwango cha juu cha utendaji na kusema kuwa mafunzo hayo yanapaswa kuwa ya ubunifu na kuzingatia mabadiliko ya haraka katika sekta ya afya.

Mwisho Bi. Ziada alitoa wito kwa wadau wote katika sekta ya afya kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa miongozo inayoundwa inatekelezwa kikamilifu na kwa ufanisi kwani itasaidia kufikia lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote.