Ministry of Health

TUTUMIE MITANDAO YA KIJAMII KUHABARISHANA TAARIFA ZA TAHADHARI, KINGA DHIDI YA EL NIÑO NA EBOLA ‎

Posted on: September 23rd, 2026

‎Na WAF – SHINYANGA.
‎
‎Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amewataka wakazi wa Kishapu na wananchi kwa ujumla,  kutumia WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii kuhabarishana kuhusu tahadhari, kinga na hatua za kuchukua dhidi ya mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola (EVD), ili kuwawezesha wananchi kujikinga na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
‎
‎Mhe. Masindi amesema hayo Septemba 23, 2026 wakati akizungumza na timu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na wadau mbalimbali wa maendeleo  waliofika mkoani humo kwa ajili ya kufanya Uelimishaji, Uhamasishaji na Ushirikishwaji wa jamii wakati wa dharura za mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola (EVD).
‎
‎Ameeleza kuwa  kwa sasa kaya nyingi zina angalau simu moja yenye matumizi ya WhatsApp, hali inayowezesha tahadhari, kinga na hatua za kuchukua dhidi ya mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola (EVD) kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.
‎
‎“Kila kaya kama ina watu wawili, watatu basi kuna simu moja ya WhatsApp ndani ya familia hiyo. Sasa simu hizi zimekuwa ni msaada mkubwa sana kufikisha taarifa ambazo ni sahihi za kinga na hatua za kuchukua dhidi ya mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola (EVD) na zikaweza kusaidia sana kuiokoa jamii kwa ukubwa zaidi,” Alisisitiza Mhe. Masindi.
‎
‎Hata hivyo ametoa mfano wa matukio ya mafuriko  kulingana na na utabiri wa mamlaka ya hali ya  hewa, amesema WhatsApp inaweza kusaidia tahadhari dhidi ya madhara yatokanayo na  mvua za El Niño ,Hivyo taarifa hizo kuwafikia wananchi kwa haraka na kutawezesha kuchukua hatua mapema.
‎
‎Aidha, amesisitiza matumizi sahihi  ya mitandao ya kijamii itawezesha kuelimishana  Umma kuhusu kinga dhidi ya Ugonjwa wa Ebola (EVD) na hatua za kuchukua, huku akiwataka wananchi kufuatilia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika na kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa zinazoweza kusababisha hofu na mkanganyiko.
‎

‎ Amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na maelekezo kutoka vyanzo rasmi kuhusu tahadhari, kinga na hatua za kuchukua dhidi ya mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola (EVD).