Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TUKATE BIMA YA AFYA KWA UHAKIKA WA MATIBABU.

Posted on: September 1st, 2024

Na WAF -  Mtwara

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewaomba wananchi Mkoani Mtwara kukata Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa matibabu na huduma bora za afya pindi wanapougua.


Prof. Nagu amesema hayo leo Septemba 2, 2024 wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliyopo Mkoani Mtwara na kisha kuzungumza na baadhi ya watumishi mara baada ya ziara yake ya kujionea maendeleo ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo.


Prof. Nagu amewaomba wananchi hao kutenga fedha wakati wa mavuno ya mazao yao kwa ajili ya kukata Bima ili kuwa na uhakika wa matibabu


Amesema uwepo wa vifaa Tiba vya kisasa hospitalini hapo umegharimu fedha nyingi hivyo ni vyema wananchi wakate bima ili kusaidia shughuli za uendeshaji wa Hospitali na kuendelea kupata huduma bora.


"Kulipia matibabu ya papo kwa papo ni changamoto Tunaomba tunapovuna mazao yetu korosho, mbaazi tujitahidi sana kuwekeza tununue bima, kila mtu akiwa na bima hatutakuwa na changamoto, unaingia tu hospitali unapata matibabu" amesema Prof. Tumaini. 


Pia amewasihi Watumishi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini  kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo.



"Ili Hospitali iendelee kuwa na wateja wengi ni lazima watumishi watoe huduma bora kuanzia lango kuu la kuingilia na kuzingatia lugha za staha na muda sahihi wa kupata huduma" amesema Prof. Nagu.


Sambamba na hilo, Prof Nagu ameuomba uongozi wa Hospitali hiyo kutumia mbinu mbalimbali zitakazosaidia kujitangaza ikiwa ni pamoja na kuweka kambi za matibabu ili kuendelea kuweka imani kwa wananchi wa ukanda wa Kusini.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti ndugu wa wagonjwa waliofika kupata huduma Hospitalini hapo wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wa Hospitali hiyo kwani kwa sasa imekuwa tegemezi kubwa kwa wananchi wa ukanda wa Kusini na nchi jirani kama vile Msumbiji na Visiwa vya Comoro.